MALI-SIASA-USALAMA

Mali: Imam Dicko atoa wito wa utulivu baada ya machafuko mapya Bamako

Vizuizi vimewekwa karibu na msikiti ambapo Imam Dicko aliongoza sala kwa waathiriwa wa machafuko ya siku mbili zilizopita huko Bamako.
Vizuizi vimewekwa karibu na msikiti ambapo Imam Dicko aliongoza sala kwa waathiriwa wa machafuko ya siku mbili zilizopita huko Bamako. MICHELE CATTANI / AFP

Imam Mahmoud Dicko, kiongozi mkuu wa maandamano na mkosoaji mkubwa wa Rais Ibrahim Boubacar Keita ametoa wito wa utulivu baada ya siku mbili za machafuko katika maandamano dhidi ya rais wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na ripoti ya mwisho machafuko hayo yamesababisha vifo vya watu 11 tangu siku ya Ijumaa.

Kati ya Ijumaa na Jumapili alasiri, machafuko hayo yamesababisha watu 1 kupoteza maisha na wengine 124 kujeruhiwa, kulingana na ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa chanzo cha hospitali.

Hata hivyo machafuko hayo yalipunguka siku ya Jumapili, ingawa hali bado ni tete katika baadhi ya maeneo.

Shughuli mbalimbali zimezorota kwa siku kadhaa kutokana na vizuizi ambavyo vimewekwa barabarani.

Mahakama moja na ofisi ndogo ya chama tawala vimeharibiwa katika Wilaya ya 5 katika mji mkuu wa Mali, Bamako.Na katika kitongoji cha Badalabougou, kulikoshuhudiwa machafuko siku ya Jumamosi jioni, mamia ya watu walihudhuria mazishi ya watu wanne waliouawa siku moja kabla. Baada ya mazishi, waandamanaji walirudisha vizuizi barabarani na milio ya risasi ilisikika.

Waandamanaji wameshtumu vikosi vya ulinzi kwamba viliua watu kadhaa kwa kuwapiga risasi.

"Vikosi vya jeshi ndio vilianza kuwafyatulia risasi raia. Tumekuwa na vifo vingi hapa. Kama wangesikiliza raia, hali hii haingetokea. Lakini mapambano yanaendelea, na huu ni mwanzo wa mapambano, " amesema mmoja wa waandamanaji hao.