MALI-SIASA-USALAMA

Taasisi nne za kimataifa zalaani machafuko ya Bamako na zatoa wito wa mazungumzo

Waandamanaji katika wilaya ya Badalabougou huko Bamako Jumapili Julai 12, 2020.
Waandamanaji katika wilaya ya Badalabougou huko Bamako Jumapili Julai 12, 2020. MICHELE CATTANI / AFP

Wawakilishi wa Umoja wa Afrika, jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wanasema wana wasiwasi kuhusu machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mali, na wametoa wito wa utulivu.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu wiki hii, wawakilishi wa taasi hizo nne wamesema "wa wasiwasi mkubwa " na "wanalaani vikali aina yoyote ya machafuko kama njia ya kusuluhisha mgogoro".

Pia "wanalaani" matumizi ya nguvu ya vikosi vya usalama, "na wametoa wito kwa pande zote kujizuia na machafuko na wameomba kutia mble mazungumzo kila wakati".

Wamebaini kwamba kukamatwa kwa viongozi wa maandamano kunazuia mazungumzo haya, ambayo hata hivyo yalipendekezwa na Rais Ibrahim Boubacar Keïta.

Mji mkuu wa Mali umeendelea kukumbwa na machafuko, tangu siku ya Ijumaa. Machafuko ambayo yalisababisha vifo vya watu 11 na wengine 124 kujeruhiwa, kulingana na afisa wa wodi ya dharura katika hospitali kukuu katika mji mkuu wa Mali.

Hayo yanajiri wakati Imam Mahmoud Dicko, kiongozi mkuu wa maandamano na mkosoaji mkubwa wa Rais Ibrahim Boubacar Keita ametoa wito wa utulivu baada ya siku mbili za machafuko katika maandamano dhidi ya rais wa nchi hiyo.