Mali: Viongozi wa maandamano waachiliwa huru
Imechapishwa:
Baada ya machafuko makubwa kushuhudiwa huko Bamako mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wa upinzani dhidi ya Rais wa Mali IBK waliokamatwa katika siku za hivi karibuni, hatimaye wameachiliwa wako huru tangu Jumatatu Julai 13.
Hata hivyo hali bado ni tete katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bamako.
"Wateja wangu, Choguel Maïga, Kaou Djim na wengine wote wameachiliwa huru," mmoja wa wanasheria wao, wakili Alifa Habib Koné amesema.
Taarifa hiyo imethibitishwa na mmoja wa wanasheria wenzake. Mamlaka nchini Mali wanajaribu kutuliza mvutano huo. Kwa sababu baada ya viongozi wa upinzani, wafuasi wao 21waliokuwa wanazuiliwa wameachiliwa huru.
Imam Oumarou Diarra, ni miongoni mwa viongozi wa upinzani dhidi ya rais Ibrahim Boubacara Keita walioachiliwa huru. Alikuwa akiongoza sala kuu ya Ijumaa katika uwanja wa Uhuru Ijumaa Julai 10, siku ya maandamano ya vuguvugu la M5, kabla ya kwenda kuhamasisha waandamanaji waliokusanyika katika ua wa shirika la utangazaji la ORTM. Hapo ndipo maafisa wa polisi walimkamata, amesema kiongozi wa tume ya maandalizi na uhamasishaji ya vuguvugula CMAS la Imam Dicko.
"Usiku wa kwanza ulikuwa mgumu kidogo, kwa sababu hakukuwa na kitanda, hakukuwa na umeme, na hakukuwa na choo katika chumba nilikokuwa nilizuiliwa. Nilipofika, walinihoji bila wakili wangu. Nilikamatwa kuhusiana na uwepo wa waandamanaji katika majengo ya umma, " zmesemz Imam Dicko.
Mapema wiki hii Imam Mahmoud Dicko alitoa wito wa utulivu baada ya siku mbili za machafuko katika maandamano dhidi ya rais wa nchi hiyo.