AFRIKA KUSINI-CORONA-AFYA

Coronavirus: Afrika Kusini yaongoza kwa maambukizi barani Afrika

Wahudumu wa afya waandamana wakidai kupewa vifaa na uwezo zaidi wa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19. Juni 19, 2020.
Wahudumu wa afya waandamana wakidai kupewa vifaa na uwezo zaidi wa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19. Juni 19, 2020. REUTERS/Mike Hutchings

Idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Afrika Kusini sasa imefikia zaidi ya Laki tatu, na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa mataifa 10 yanayoongoza kwa maambukizi duniani.

Matangazo ya kibiashara

Barani Afrika, Afrika Kusini inaoongoza kwa maambukizi na jana watu wengine Elfu 12 walipatikana na virusi hivyo.

Watu 12,757 wameambukizwa virusi vya Corona katika muda wa saa 24 zilizopita na kufanya nchi hiyo kuwa na visa 311,000 vya maambukizi.

Afrika Kusini imerekodi vifo vipya 107 katika muda wa saa 24 zilizopita na kufanya jumla ya idadi ya vifo kufikia 4,453, kulingana na takwimu za Chuo Kikuu cha cha Johns Hopkins.

Watu zaidi ya Milioni 2.3 wamepimwa tangu mwezi Machi nchini humo.

Afrika Kusini ilirejesha tena masharti ya watu kutotembea na kuzuia uuzwaji wa pombe, baada ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona kuendelea kushuhudiwa nchini humo.

Hivi karibuni Rais Cyril Ramaphosa aliwaonya raia wake kwamba serikali imetekeleza jukumu lake na sasa raia ndio wana kazi kubwa ya kufanya kuhusu kujikinga na ugonjwa huo hatari.