MISRI-LIBYA-USALAMA

Bunge la Misri laidhinisha jeshi kupelekwa nchini Libya

Bunge la Misri limeruhusu jeshi la nchi hiyo kutumwa nchini Libya kukabiliana na makundi ya 'kigaidi'.
Bunge la Misri limeruhusu jeshi la nchi hiyo kutumwa nchini Libya kukabiliana na makundi ya 'kigaidi'. REUTERS/Mohamed Abd El Ghany

Bunge la Misri limeidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi  wake nchini Libya, baada ya Rais Abdel Fattah al-Sisi kutishia kutuma jeshi la nchi yake nchini humo kupambana na kile alichosema ni magaidi na kulinda maslahi ya nchi yake.

Matangazo ya kibiashara

Bunge la Misri limesema hatua hiyo ya kupelekwa kwa wanajeshi nje ya mipaka ya Misri itasaidia kulinda usalama wa kitaifa wa Misri dhidi ya wanamgambo wenye silaha za kihalifu na magaidi.

Upigaji kura huo uliofanyika Jumatatu wiki hii, katika bunge lililokuwa limejaa wafuasi wa Rais Sisi, zoezi ambalo lilifanyika faraghani ambapo wabunge walijadili "vitisho vinavyolikabili taifa kutoka eneo la magharibi, ambapo Misri inachangia mpaka wa jangwa na Libya, eneo lililokumbwa na vita.

Hatua hiyo ya upigaji kura imekuja siku moja baada ya rais wa Misri kukutana na baraza la ulinzi la kitaifa ambalo linajumuisha spika wa Bunge, waziri wa ulinzi, waziri wa mambo ya nje na makamanda wa jeshi.

Rais Sisi alionya kwamba maendeleo ya vikosi vya serikali ya Tripoli (GNA) inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, Magharibi mwa Libya katika mji wa Sirte yangechochea uingiliaji kijeshi wa Misri.

Serikali inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa (GNA) iliita onyo hilo kama 'tamko la vita'.