Coronavirus: WHO yaonya mataifa mengi barani Afrika huenda yakapata maambukizi zaidi
Shirika la Afya Duniani WHO linasema linahofia ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona barani Afrika, huku likionya kuwa kuendelea kushuhudiwa kwa ongezeko hilo hasa nchini Afrika Kusini, huenda hatua hiyo ikaathiri mataifa mengine barani Afrika.
Imechapishwa:
Bara la Afrika limeshuhudia vifo vya watu Elfu 15 na wengine zaidi ya Laki Saba na Elfu 25, wamemabukizwa virusi vya janga hilo hatari.
Kufikia sasa ugonjwa wa Covid-19 umesababisha vifo vya watu 608,000 duniani, huku visa Milioni 14.6 vya maambukizi vikithibitishwa na wagonjwa Milioni 8.2 wakithibitishwa kupona ugonjwa huo.
Wataalam waliobobea wanaendelea kutafuta chanjo ya ugonjwa huo ili kuweza kunusuru afya za binadamu na uchumi ambao umedorora kwa kiasi kikubwa katika nchi mbalimbali duniani kufuatia masharti yaliyowekwa na nchi hizo kwa kupambana dhidi ya ugonjwa huo ambao ulianza huo Wuhan, nchini China, mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana.
Marekani ndio inaendelea kuongoza kwa idadi kubwa ya maambukizi duniani ikifuatia na Brazil.
Barani Afrika, Afrika Kusini ndio inaongoza kwa idadi kubwa ya maambukizi.