COTE D'IVOIRE-GBAGBO-USALAMA-SIASA

Côte d'Ivoire: Chama cha FPI chamuomba Gbagbo kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa Oktoba

Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, Januari 15, 2019.
Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, Januari 15, 2019. © Peter Dejong

Chama cha rais wa zamani wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo, FPI kimemtaka rais huyo wa zamani kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Haijajulikani mpaka sasa ikiwa Gbagbo atafuata pendekezo la chama chake na kurudi nchini Côte d'Ivoire.

Lakini, kuwania kwa Gbagbo, ambaye alikataa kujiuzulu baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 kupingwa, na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyogharimu maisha ya watu 3,000 , kunaibua maswali mengi nchini humo, ambapo baadhi wana hofu ya kutokea machafuko mapya.

Uchaguzi wa Oktoba 31 unaonekana kama kipimo kwa utulivu wa nchi.

Laurent Gbagbo aliachiliwa huru mwaka jana na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) katika kesi yake ya uhalifu dhidi ya binadamu na kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji.

Naye Marcel Amon-Tanoh, aliyekuwa mshirika wa rais wa sasa Alassane Ouattara na Waziri wa zamani wa Mambo ya nje, siku ya Jumatano alitangaza kuwa atawania katika uchaguzi huo wa rais wa mwezi Oktoba.

Hayo yanajiri wakati rais anayemaliza muda wake nchini humo Alassane Ouattara anaendelea kupata shinikizo la kuwania kwenye kiti cha urais, siku chache baada ya kifo cha waziri mkuu Amadou Gon Coulibaly.

Wiki hii rais Ouattara alipata ridhaa ya wabunge kutoka chama chake kuwani kiti cha urais katika uchaguzi huo.