DRC-USALAMA

Maeneo ya Mashariki mwa DRC yaendelea kukumbwa na ukosefu wa usalama

Askari wa kikosi cha Umoja aw Mataifa kutoka India wakipiga doria katika eneo la Ntoto huko Walikale.
Askari wa kikosi cha Umoja aw Mataifa kutoka India wakipiga doria katika eneo la Ntoto huko Walikale. MONUSCO/ Lt Col Kuldeep Kumar

Watu zaidi ya 30 wameuwa na mamia kuyakimbia makawao siku chache zilizopita, baada ya kutokea kwa mapigano kati ya wapiganaji wa kundi la waasi wa NDC katika Wilaya ya Walikale, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo wanajeshi watatu wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo wameuawa, mmoja akijeruhiwa vibaya baada ya waasi wa kundi la M23 kuwashambulia eneo la Rutshuru, karibu na Hifadhi ya wanyama ya virunga, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kwa mjibu wa mamlaka eneo hilo, mapigano makali yalishuhudiwa kwa muda kati ya jeshi la serikali, FARDC, na waasi hao wa M23.

Maeneo ya Mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yameendelea kushuhudia ukosefu wa usalama. Makundi yenye silaha yanaendelea kutekeleza vitendo viovu dhidi ya raia, hususa mauaji, ubakaji, na uporaji wa mali za wakazi wa maeneo hayo.

Mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yanaendelea kukaliwa na makundi hayo na kusababisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao na kukimbilia maeneo salama.

Hivi karibuni jeshi la nchi hiyo, FARDC, lilianzisha operesheni ili kuyatokomeza makundi hayo, huku baadhi ya wapiganaji wakijisalimisha kufuatia wito wa Rais Felix Tshisekedi unaowataka kuweka silaha chini na kujiunga na mchakato wa amani.