Mali: Marais watano wa Afrika Magharibi wawasili Bamako kujaribu kusuluhisha mzozo wa kisiasa
Marais wa Niger, Nigeria, Senegal, Côte d'Ivoire na Ghana watajaribu, baada ya ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, kupata suluhisho la mzozo ambao unaendelea kuikumba Mali kwa wiki sita sasa.
Imechapishwa:
Rais wa Côte d'Ivoire Alassane Ouattara ndiye wa kwanza ambaye ndege yake ilitua katika uwanja wa ndege wa mjini Bamako, Julai 23, 2020. Mwenzake wa Senegal, Macky Sall pia aliwasili, huku akivalia barakoa usoni mwake kwa kujikinga na maambukizi ya Covid-19. Muda mchache baadaye rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, Mahamadou Issoufou wa Niger na Nana Akufo-Addo wa Ghana waliwasili. Wote wamepokelewa na mwenyeji wao rais Ibrahim Boubacar Keita kwenye uwanja wa ndege.
Upinzani wataka waziri mkuu ajiuzulu
Marais hao watano watakuwa mjini Bamako kwa saa kadhaa kusaidia kumaliza mzozo wa kisiasa unaoikumba nchi ya Mali. Ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), ambao ulikuwa mjini Bamako hivi karibuni, ulitoa msimamo wake: hakuna kusikia madai ya upinzani kuhusu kujiuzulu kwa rais Ibrahim Boubacar Keïta, madai yaliyotolewa na upinzani.
Marais hao watano watashikilia msimamo huo. Lakini, kufikia sasa upinzani hautilii tena manani madai hayo. Katika waraka ambao RFI ilipata kopi, upinzani unataka Waziri Mkuu Boubou Cissé, ajiuzulu. "Ni suala lisilojadiliwa," amesema mmoja kati ya wanasiasa wa upinzani.
Mkutano na Imam Dicko
Kulingana na vyanzo kutoka nchini Mali, marais hao wanatarajia kwanza kukutana na mwenzao, rais Ibrahim Boubacar Keïta, kabla ya kukutana, baada ya chakula cha mchana, na Imam Dicko, kiongozi mwenye ushawishi mkubwa anayeongoza maandamano kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. Ataambatana na viongozi kadhaa wa upinzani, ikiwa ni pamoja na waziri wa zamani katika utawala wa Ibrahim Boubacar Keita, Choguel Maïga, mwenyekiti wa kamati ya vuguvugu ya M5.
Lengo la marais hao ni kujaribu kupatanisha pande zinazokinzana nchini Mali, lakini suala hilo bado ni ndoto kulifika, kwa sababu mgogoro wa kisiasa na mgogoro wa baada ya uchaguzi bado haujatatuliwa.
Kwanza, kuna maswala ya kitaasisi na ya uchaguzi. Wiki iliyopita, ujumbe wa ECOWAS ulipendekeza kwamba wajumbe wapya wa Mahakama ya Katiba wateuliwe haraka. Lakini wiki hii, uteuzi wao ulijikuta unakabiiliwa vizuizi na vikwazo vya sheria pamoja na ukosefu wa taaluma. Itakumbuka kwamba, majaji hao wapya, ndio wanastahili kusuluhisha mzozo wa uchaguzi, ambao ni miongoni mwa masuala yanayosababisha mgogoro huo wa kisiasa unaoendelea nchini Mali.
Pia kuna maswala zaidi ya kisiasa. ECOWAS ilipendekeza kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, kwani Mali haina mawaziri kwa karibu siku 40 sasa.