LIBYA-MAPIGANO-USALAMA

Marekani: Urusi inaingilia kijeshi Libya kupitia mamluki wa Wagner

Picha hii, ambayo AFP ilipata kutoka Africom Julai 15, 2020, inaonyesha bomu la kutegwa ardhini katika eneo la makazi la Tripoli.
Picha hii, ambayo AFP ilipata kutoka Africom Julai 15, 2020, inaonyesha bomu la kutegwa ardhini katika eneo la makazi la Tripoli. Handout / AFRICOM / AFP

Marekani imeishutumu Urusi kwa kuingilia kijeshi nchini Libya kupitia mamluki wa kundi la Wagner; Kwa mujibu wa Marekani hatua hiyo ya Urusi ni katika kupeleka vifaa vya kijeshi na hivyo kukiuka vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa nchini Libya.

Matangazo ya kibiashara

Katika wiki za hivi karibuni, Marekani ilitoa taarifa kadhaa zinazoishtumu Urusi kuchochea vita nchini Libya. Madai ambayo Kremlin imekuwa ikikanusha.

Picha za satelaiti ziliyotolewa na Pentagon, zinaonyesha ndege kadhaa za kivita, magari ya kijeshi yakisheni makombora, vifaru ambavyo vinaweza kuhimili milipuko ya mabomu. Picha ambazo zilinaswa huko Sirte na kwenye kambi ya kikosi cha anga cha Al-Khadim mashariki mwa Libya.

Marekani imebaini kwamba vifaa hivyo vya kijeshi vimetumwa kwa kundi la Wagner, kundi la kibinafsi la mamluki wa kukodiwa kutoka Urusi ambalo linajulikana kuwa na ukaribu na rais Vladimir Putin na linapigana nchini Libya kwa kumsaidia Marshal Khalifa Haftar, mbabe wa kivita huko Mashariki mwa Libya, ambaye amekuwa akijaribu kuudhibiti mji wa Tripoli kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, mamluki hawa ni wengi nchini Libya. Na wiki iliyopita, Africom, makao makuu ya Marekani barani Afrika, yalilishtumu kundi la Wagner kwa kutega mabomu ya ardhini katika mji wa Tripoli na viunga vyake.

Picha hii ya satelaiti, ambayo AFP ilipata kutoka Africom, inaonyesha vifaa ambavyo Urusi ilikabidhi kundi la Wagner, kulingana na taarifa za ujasusi za Marekani, kwenye kambi ya Al-Khadim, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita na makombora
Picha hii ya satelaiti, ambayo AFP ilipata kutoka Africom, inaonyesha vifaa ambavyo Urusi ilikabidhi kundi la Wagner, kulingana na taarifa za ujasusi za Marekani, kwenye kambi ya Al-Khadim, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita na makombora US Africa Command / AFP

Katika taarifa, Africom imebaini kwamba "Urusi inatumia kundi la Wagner nchini Libya kuanzisha uwepo wake wa muda mrefu katika Bahari ya Mediterranean".

Hadi sasa, Moscow imekuwa ikikana tuhuma hizi. Lakini Washington, inasema "Urusi inahusika katika vita nchini Libya na Kremlin inadanganya kila wakati itakapokanusha."