ECOWAS yatiwa wasiwasi na mzozo wa kisiasa nchini Mali
Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, wanakutana kujadili mzozo wa kisiasa nchini Mali, baada ya jitihada za hapo awali kutozaa matunda.
Imechapishwa:
Lengo la mazungumzo hayo ni kutafuta mbinu za kusuluhisha mzozo kati ya rais Ibrahim Boubacar Keita na upinzani unaomtaka rais huyo kujiuzulu, huku Mwenyekiti wa ECOWAS na rais wa Niger Mahamadou Issoufou akiwataka viongozi wenzake kuchukua hatua nzito dhidi ya hali ya kisiasa nchini Mali.
Wiki iliyopita viongozi wa ECOWAS walitoa mapendekezo ya kutaka kuundwa kwa serikali mpya na kuwashirikisha wapinzani na viongozi wa masharika ya kiraia, mependekezo ambayo yamekataliwa na upinzani.
Hii inakuja baada ya marais watano kutoka nchi za ECOWAS kukutana Alhamisi wiki iliyopita na wadau mbalimbali wakiwemo rais Ibrahim Boubakar Keita, wawakilishi wa upinzani na mashirika ya kiraia kujaribu kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Mali, huku kinara wa Upinzani Imam Mahamoud Dicko akisema hakuna hatua chanya yoyote imefikiwa na kwamba watu waliopoteza maisha hawawezi kufia bure.
Madai ya upinzani ni kuona rais Ibrahim Boubakar Keita anajiuzulu, jambo ambalo ECOWAS inasema ni kinyume na demokrasia.