MALI-USALAMA

Mali yawapoteza askari wake watano katika mashambulio mawili

Askari wa Mali wakipiga doria karibu na kingo za Mto Niger.
Askari wa Mali wakipiga doria karibu na kingo za Mto Niger. Reuters

Wanajeshi watano wa Mali wameuawa na wengine watano kujeruhiwa Katika mashambulio mawili ya wakati mmoja yaliyotekelezwa usiku wa kuamkia leo Jumatatu na wanajihadi katikati mwa nchi hiyo, maafisa wa jeshi la Mali wamesema.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa Twitter wa jeshi hilo la Mali ni kuwa mashambulio hayo mawili ya wakati mmoja yalifanyika usiku wa maanane kuamkia leo jumatatu ya agosti tatu kwenye miji ya Goma-Coura na Diabaly, ambapo wapiganaji wa kigaidi walianza kwa kuzishambulia kambi hizo kwa silaha za rashasha na silaha nzito, maafisa wa jeshi la Mali wamebainisha.

Chanzo cha kijeshi kimesema hadi kufikia asubuhi hii miili ya wanajeshi watano ndio imepatikana huku wanajeshi wengine watano waliojeruhiwa wanaendelea kupewa matibabu ya dharura.

Maafisa wa usalama wamefahamisha kuwa opairesheni kabambe ya kuwasaka wanajihadi hao inaendelea kwenye maeneo hayo huku wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa mataifa, Minusma wakiwa wameshirikishwa katika operesheni hizo.