DRC-SIASA-USALAMA

DRC: Makabiliano yatokea kwenye mpaka na Zambia baada ya mauaji ya mfuasi wa UDPS

Malori yakiegesha katika moja ya maeneo huko Kasumbalesa (Februari 2016), kwenye mpaka na Zambia.
Malori yakiegesha katika moja ya maeneo huko Kasumbalesa (Februari 2016), kwenye mpaka na Zambia. AFP PHOTO / MARC JOURDIER

Mtu mmoja amepoteza maisha na majengo kuharibiwabaada ya wafuasi wa chama cha UDPS cha rais Felix Tshisekedi kuandamana katika mji wa Kasumbalesa, Kusini Mashariki mwa nchi hiyo, kulalamikia utovu wa usalama.

Matangazo ya kibiashara

Meya wa mji wa Kasumbalesa kwenye eneo la mpaka wa DRC na Zambia, André Kapampa, amefahamisha kuwa mfuasi huyo wa chama tawala nchini DRC cha UDPS aliuawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa wamejihami kwa silaha, baada ya kutokea mvutano kati yao, na kwamba vikosi vya usalama jeshi ama polisi hawahusishwi na kifo hicho.

Hata hivyo, vyanzo mbalimbali vimebaini kwamba mtu huyo ameuawa na mmoja wa maafisa wa usalama.

Wafuasi wanaomuunga mkono rais Felix Tshisekedi waliandamana kwenye mji huo wa Kasumbalesa karibu na mpaka na Zambia ambapo inadaiwa kuwa walivunja majengo kadhaa ya serikali kupinga ongezeko la visa vya  uhalifu katika eneo hilo la Kusini Mashariki mwa DR Congo.

Katika tangazo lake kwa vyombo vya habari, chama cha UDPS kimefahamisha kuwa watu wawili waliuwawa wakati wa maandamano, huku wengine wanane wanashikiliwa na polisi kwenye mji huo wa Kasumbalesa.