MAREKANI-LIBYA-USALAMA-SIASA

White House yalaani uwepo wa majeshi ya kigeni nchini Libya

Majeshi yanayoongozwa na Marshal Khalifa Haftar, huko Bengazhi. (picha ya kumbukumbu.
Majeshi yanayoongozwa na Marshal Khalifa Haftar, huko Bengazhi. (picha ya kumbukumbu. Abdullah DOMA / AFP

Ikulu ya White House nchini Marekani, imekashifu vikali kuwepo kwa majeshi ya mataifa mengine nchini Libya, ikihofu kuwa hali hiyio itazidisha mzozo uliopo.

Matangazo ya kibiashara

Mshauri wa maswala ya usalama wa rais Donald Trump Robert C. O'Brien amesema ushindani wa kiubabe kati ya mataifa mbali mbali nchini Libya ni tishio kubwa la kiusalama.

Hayo yanajiri wakati makabiliano makali yametokea kati ya wanamgambo kufuatia kukamatwa kwa mamluki kadhaa kutoka Chad ambao ni sehemu ya "kundi la wahalifu" ambao "wamekuwa wanajihusisha na visa vya wizi na uporaji", kulingana na mamlaka nchini Libya.

Mamluki hao walikuwa chini ya uongozi wa Osama Jouili, mkuu wa vikosi vya majeshi Magharibi mwa Libya. Agizo la kuwakamata lililotolewa na Fathi Bachagha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNA). Wawili hao ambao ni kutoka kambi moja ya kisiasa wako katika upinzani mkubwa.

Hii sio mara ya kwanza tofauti kati ya wanamgambo kutoka Magharibi mwa Libya kuzuka. Hii ilitokea mara kadhaa hapo awali, wakati na baada ya kushindwa kwa mashambulizi ya Mashal Khalifa Haftar ya kutaka kuuteka mji mkuu Tripoli.

Kulingana na ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa, wanamgambo nchini Libya sasa ni kama makundi, ambayo kila upande unatetea masilahi yake na kutafuta kunufaika kupitia mapato ya serikali wakati ukitumia udhaifu wake na ufisadi mkubwa uliokithiri.