DRC-UN-MAUAJI

Ripoti: Watu zaidi ya 1,300 wauawa tangu Januari hadi Juni 2020 DRC

Visa vingi vya mauaji vimeripotiwa katika eneo la Beni, mkoani Kivu Kaskazini na katika mkoa wa Ituri.
Visa vingi vya mauaji vimeripotiwa katika eneo la Beni, mkoani Kivu Kaskazini na katika mkoa wa Ituri. Photo MONUSCO/Force

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema zaidi ya watu 1,300 wameuawa nchini DRC tangu mwezi Januari hadi juni mwaka huu wa 2020 na vikosi vyenye silaha hii ikiwa ni mara tatu zaidi ukilinganisha na mwaka uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya Umoja wa mataifa iliyochapishwa hapo siku ya Jumatano inasema wapiganaji kutoka kwa vikosi vya wapiganaji wenye silaha huko Mshariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vimehusishwa katika mauaji ya watu wasiopungua elfu moja mia tatu kumi na watano, miongoni mwao wanawake 267 na watoto mia moja sitini na watano.

Umoja aw Mataifa inasema hii ni mara tatu zaidi ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, idadi hii huenda ikaongezeka kufuatia vitendo vya uhalifu, ubakaji na unyanyasaji unaofanyiwa wananchi sio tu na makundi ya wapiganaji lakini pia jeshi la polisi, maafisa wa usalama na jeshi la serikali ya DRC.

Matukio ya ubakaji yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kupitia ripoti za Umoja wa Mataifa yakitajwa kuwa ni uhalifu siyo tu kwa mujibu wa sheria za DRC bali pia sheria za kimataifa.