COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA

Rais Ouattara kuwania kiti cha urais katika uchaguzi ujao

"Nitawania kiti cha urais katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 31," ametangaza Alassane Ouattara.
"Nitawania kiti cha urais katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 31," ametangaza Alassane Ouattara. SIA KAMBOU/AFP

Rais wa Cote d’ Ivoire Alassane Ouattara, mwenye umri wa miaka 78, hatimaye ameweka wazi msimamo wake kuwa atagombea kwa muhula wa tatu, hatua ambayo imekuja baada ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wake Amadou Gon Coulibaly Julai 8.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo hatua ya rais Ouattara kugombea tena urais katika uchaguzi wa mwezi Oktoba imekosolewa na wapinzani nchini humo.

Katika hotuba yake kupitia runinga ya taifa Alhamisi ya wiki hii, rais Ouattara amefahamisha kuwa hakuwa na chaguo lingine, baada ya kuhoji dhamiri zake.

Ouattara amefikia uamuzi huo baada ya kushinikizwa na chama chake, wabunge kutoka chama chake na taasisi mbalimbali katika chama cha RHDP

kumtaka apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao, baada ya kifo cha waziri mkuu Amadou Gon Coulibaly hivi karibuni ambaye alikuwa mrithi wake.

Miezi michache iliyopita, Rais wa Cote d'Ivoire alisema hatowania katika uchaguzi wa urais ujao na kuachia nafasi kwa kizazi kipya kuliendeleza taifa hilo la Afrika, lakini kifo cha Waziri Mkuu Amadou Gon Coulibaly ambaye alikuwa aliteuliwa kupeperusha bendera ya chama tawala katika uchaguzi wa urais, kilibadili hali ya mambo.