ZIMBABWE-HRW-SIASA-USALAMA

Zimbabwe kukabiliana na wanaoipaka tope

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa .
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa . REUTERS/Philimon Bulawayo

Zimbabwe ipo mbioni kupitisha sheria mpya ambayo itatoa adhabu kali kwa vyama vya kisiasa vinavyofanya kampeni za kuharibu jina la nchi hiyo. Hatua ambayo inakosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Hii inakuja siku kadhaa baada ya rais Emmerson Mnangagwa kuvishtumu vyama vya upinzani kwa kushirikiana na mabalozi wa nchi za magharibi kuhujumu uchumi na kuchochea vitendo vya kigaidi.

Wakati huo huo shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limezitolea mwito nchi za Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, kukemea hadharani ukandamizaji uliofanywa na serikali ya Zimbabwe dhidi ya maandamano ya amani ya kupinga ufisadi yaliyofanyika Julai 31.

Shirika hilo pia limelaani kamata kamata ya kiholela dhidi ya wapinzani nchini humo.

Katika ripoti yake iliyochapishwa wiki hii, Human Rights Watch inasema kuwa serikali ya Zimbabwe imewakamata kuhusiana na maandamanano hayo, watu wasiopungua 60, ikiwa ni pamoja na mwandishi wa vitabu Tsitsi Dangarembga na msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC Fadzayi Mahere.

Ripoti hiyo ya Human Right Watch inaorodhesha visa vya kuwakamata kinyume cha sheria wakosoaji wa serikali nchini Zimbabwe, wakiwemo mwandishi wa habari aliyetuzwa kwa kazi yake Hopewell Chin'ono, na kiongozi wa kundi la kisiasa linalotaka mabadiliko la Transform Zimbabwe, Jacob Ngarivhume.