DRC-USALAMA-HAKI

DRC: Askari aliyehusika na mauaji ya Sange akamatwa

Askari wa jeshi wa DRC, aliyehusika na mauaji ya watu kumi na wanne katika mji wa Sange siku ya Alhamisi jioni , Julai 30, 2020, yuko kizuizini tangu jana Ijumaa.

Askari wa jeshi la DRC, FARDC.
Askari wa jeshi la DRC, FARDC. John WESSELS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Zoezi la kumtafuta na kumpata askari huyo wa bataliani ya 2 ya Kikosi maalumu 12 cha jeshi lilidumu wiki, tangu atekeleze uhalifu wake katika eneo hilo la Uvira.

Askari huyo mlevi aliwafyatulia risasi watu ambao walikuwa wamekuja kuwaokoa watu wawili ambao askari huyo alikuwa amejaribu kuwapora pesa. Wakati huo watu 14 walifariki papo hapo na wengine 8 walijeruhiwa. Askari huyo alikamatwa huko Nyangezi katika eneo la Walungu. Ana umri wa miaka thelathini, alionekana amechoka kidogo, baada ya kukamatwa na vijana waliokuwa wakipiga doria usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii katika eneo linalojulikana kwa jina la "Chez Faké", karibu na eneo la biashara la Munya.

Askari huyo alikabidhiwa jeshi la DRC, FARDC, huko nyangezi, kabla ya kusafirishwa jana Ijumaa mjini Bukavu, kwa mujibu wa Firmin Bisimwa, kiongozi wa shirika la kiraia mjini Nyangezi.

Gavana wa mkoa wa Kivu Kusini, Théo Kasi Ngwabidje, amethibitisha taarifa hii kwenye ujumbe wa Twitter na kuahidi kwamba sheria itafuata mkondo wake.