DRC-M23-USALAMA

Kundi la zamani la M23 lanyooshewa kidole kuhatarisha usalama wa raia Mashariki mwa DRC

wapiganaji wa kundi la zamani la M23, Februari 2014.
wapiganaji wa kundi la zamani la M23, Februari 2014. AFP PHOTO/ ISAAC KASAMANI

Visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini DRC vimeongezeka kwa asilimia 100, huku eneo la Mashariki mwa nchi hiyo, likiendelea kushuhudia mashambulizi ya kigaidi, vyanzo vya usalama vimebaini.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo kundi la zamani la waasi la M23 limeshtumiwa kutekeleza shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi huko Rutshuru na kusababisha vifo vya watu watatu.

Katika ripoti ya kikao cha mawaziri cha Julai 31, Waziri wa Ulinzi alithibitisha rasmi kwamba wapiganaji wa M23 walifanya shambulio dhidi ya jeshi la FARDC kwenye ngome zao mnamo tarehe 22 Julai. Msemaji wa kikundi cha waasi cha M23, Élie Mutela, amekanusha madai hayo.

"Ni kweli kwamba kuna wenzetu ambao wapo katika mtaa wa Rutshuru. Lakini hawajaendesha shambulizi lolote lile dhidi ya ngome za jeshi, " Élie Mutela amebaini.

Kulingana na vyama vya kiraia katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Julai 22 "Mapigano makali yaliripotiwa, huku silaha za kivita zikitumiwa na waasi wa kundi la zamani la M23 dhidi ya ngome za jeshi katika eneo la Rutshuru pembezoni na mpaka wa Hifadhi ya wanyama ya Virunga.

"Ikiwa wapiganaji wa kundi la zamani la M23 wanasema kwamba hawajawahi kuendesha mashambulio dhidi ya ngome za jeshi, ni uwongo! Wao wenyewe wanatambua kwamba wako kwenye ardhi ya DR Congo. Tunaomba serikali ya DRC, kuwapa askari vifaa vizuri ili kuzuia harakati za maadui hawa wa amani, " amesema John Balingene, kiongozi wa mashirika ya kiraia ya Forces Vives.

Mwezi Februari 2019, Uganda iliwarudisha nchini DRC wapiganaji 70 wa kundi la zamani la M23, ikiwa ishara ya utekelezaji wa makubaliano ya kuwarudisha kwa hiari waasi wa kikundi hicho, makubaliano yaliyosainiwa mnamo mwaka wa 2013. Mchakato ambao ulishindwa kuendelea kwa miaka iliyofuata.