COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA

Côte d'Ivoire: Upinzani waomba fomu ya kuwania uchaguzi ya Alassane Ouattara iondolewe

L'opposition fait front ensemble et exige le retrait de la candidature d'Alassane Ouattara. Elle réclame également de profonds changements au sein de la CEI.
L'opposition fait front ensemble et exige le retrait de la candidature d'Alassane Ouattara. Elle réclame également de profonds changements au sein de la CEI. SIA KAMBOU / AFP

Upinzani nchini Côte d’Ivoire umekuja juu na kutaka rais wa nchi hiyo anayemaliza muda wake Alassane Ouattara asiwanie katika uchaguzi wa urais ujao.

Matangazo ya kibiashara

Miungano kadhaa ya vyama vya kisiasa iliyo na ushirikiano wa karibu na Henri Konan Bédié, Laurent Gbagbo, Guillaume Soro na Charles Blé Goudé wametoa taarifa ya pamoja, wakitaka fomu ya kuwania uchaguzi ya Alassane Ouattara iondolewe na kuomba kufanyike mabadiliko makubwa kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na kwenye orodha mpya ya wagombea urais ambayo ilitangazwa hivi karibuni.

Wiki iliyopita rais wa Cote d’ Ivoire Alassane Ouattara, mwenye umri wa miaka 78, aliweka wazi msimamo wake kuwa atawania kwenye kiti cha urais kwa muhula wa tatu, hatua ambayo imekuja baada ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wake Amadou Gon Coulibaly Julai 8.

Maurice Kakou Gikahué, katibu mtendaji wa chama cha PDCI amebaini kwamba uchaguzi wa Oktoba hauwezi kufanyika. Upinzani unaishutumu Tume Huru ya Uchaguzi (CEI) kutumiwa na baadhi ya viongozi serikalini na kufutilia mbali majina ya baadhi ya waombea kwa msaada wa shirika la Mawasiliano la Voodoo.

Wiki hii Simone Gbagbo, mke wa rais wa zamani wa Côte d’Ivoire, Laurent Gbagbo alimtaka rais Alassane Ouattara, kumsamehe mumewe wakati Côte d'Ivoire ikiuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.

Chama cha Gbagbo kimekuwa kikitaka rais huyo wa zamani kuruhusiwa kurejea nyumbani ili kuwania urais.

Hivi karibuni chama cha rais wa zamani wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo, FPI kilimtaka rais huyo wa zamani kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Lakini, kuwania kwa Gbagbo, ambaye alikataa kujiuzulu baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 kupingwa, na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyogharimu maisha ya watu 3,000 , kunaibua maswali mengi nchini humo, ambapo baadhi wana hofu ya kutokea machafuko mapya.

Uchaguzi wa Oktoba 31 unaonekana kama kipimo kwa utulivu wa nchi.

Laurent Gbagbo aliachiliwa huru mwaka jana na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) katika kesi yake ya uhalifu dhidi ya binadamu na kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji.