DRC-BURUNDI-MAUAJI-USALAMA

DR Congo: Wanyamulenge bado wanadai haki miaka 16 baada ya mauaji ya Gatumba

Baadhi ya waathirika wasema kamwe hawatoweza kusahau kilichotokea.
Baadhi ya waathirika wasema kamwe hawatoweza kusahau kilichotokea. SIMON MAINA / AFP

Wanyamulenge waishio nchini Burundi wameadhimisha kumbukumbu ya miaka 16 tangu kutokea kwa mauaji dhidi yao na kusababisha vifo vya watu 166 wakiwa kambini huko Gatumba magharibi mwa mkoa wa Bujumbura huku walionusurika wakiendelea kusisitiza haki kutendeka.

Matangazo ya kibiashara

Wanyamulenge wanaendelea kuyashtumu makundi ya wapiganaji Wamaï-maï na Palipehutu FNL kujihusisha na shambulio hio lililosababisha mauji hayo na kuwajeruhi wengine zaidia ya Mia moja.

Watu kutoka jamii hiyo mjini Bukavu katika mkoa wa Kivu Kusini, Mashariki mwa DRC, pia walikusanyika jana Alhamisi kuomba haki itendeke.

Muhamiriza Ineza Aline, mwakilishi wa waathiriwa, amezilauamu serikali za Burundi na DRC kwa kushindwa kuingilia kati ili haki itendeke na wahusika waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.

"Nimepoteza wapendwa wangu, watu katika jamii yangu, marafiki wa familia ambao waliondoka. Miaka kumi na sita baadaye, kinachosikitisha ni kwamba serikali ya DRC haisemi chochote, serikali ya Burundi haijalaani mauaji hayo, hata jamii ya kimataifa, jambo ambalo linatuumiza moyoni! Kuna ambao walisema kwamba wao ndio walihusika na mauaji haya. Tunaamini kwamba siku moja sheria itafuata mkondo wake, " amesema Muhamiriza Ineza Aline.

Mbunge wa zamani Enock Sebineza, amebaini kwamba mauaji ya Gatumba yanakumbusha matukio mengine mabaya. Kwa ukosefu wa

"Tunahisi kama tunasalitiwa na kanda nzima, na hata nchi yetu. Kwa kuwa Wanyamulenge waliuawa nje ya DRC, kisheria tunaitazama DRC, Burundi na Umoja wa Mataifa ndizo zinazoweza kuwasilisha malalamiko mahali popote, " amesema Enock Sebineza.

Maadhimisho haya yamefanyika katika muktadha wa machafuko ya kikabila katika wilaya za Fizi, Uvira na Mwenga, na ambayo yanendelea kuongeza idadi ya waathiriwa.

Waklati huo huo jamii ya Wanyamulenge imeiomba serikali ya DRC kuendelea na juhudi za mazungumzo na maridhiano kati ya jamii, na kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa DRC.

Kwa sasa shirika la Human Rights Watch linasema Burundi inapaswa kuchukua hatua, kuhakikisha waliyohusika na shambulio la Gatumba wanakabiliwa na mkono wa sheria na kutambua haki ni muhimu katika kuzuwiya ukatili zaidi.