SOMALIA-USALAMA

Somalia: Al Shabab yakiri kutekeleza shambulio katika Elite Hotel Mogadishu

Al-Shabab, ambayo ina uhusiano na kundi la al-Qaeda, wamekuwa wakiendesha mashambulizi ya ukatili nchini Somalia kwa zaidi ya muongo
Al-Shabab, ambayo ina uhusiano na kundi la al-Qaeda, wamekuwa wakiendesha mashambulizi ya ukatili nchini Somalia kwa zaidi ya muongo REUTERS/Feisal Omar

Wanamgambo wa kundi la Al Shababnchini Somalia wamekiri kuwa wao ndi wametekeleza shambulio kubwa katika hoteli maarufu huko Mogadishu, inayotembelewa na maafisa wa serikali, na kuwauwa raia kumi na afisa mmoja wa polisi, kulingana na ripoti rasmi iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Washambuliaji walilipua bomu lililotegwa ndani ya gari nje ya hoteli hiyo Jumamosi usiku kabla ya kuivamia na kuwateka nyara watu.

Ilichukua saa nne ili vikosi vya usalama viweze kupata udhibiti wa Elite Hotel, hoteli maarufu iliyojengwa kwenye pwani ya Lido inayotembelewa mara kwa mara na viongozi wa Kisomali.

Shambulio hilo lilitekelezwa na wanamgambo watano mapema jioni, Ismael Mukhtaar Omar, msemaji wa Wizara ya Habari ameliambia shirika la habari la AFP. "Watu kumi wameuawa, pamoja na washambuliaji watano na afisa mmoja wa polisi, " amebaini.

Wakati huo watu 250, raia lakini pia wanasiasa na wabunge, waliokuwa katika hoteli hiyo waliondolewa. Abdirasak Abdi, afisa mwandamizi katika wizaya ya habari ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo.

Hata hivyo Vikosi maalumu vya Somalia vinasema vimemaliza uvamizi huo.

Vikosi vya usalama viliizingira hoteli hiyo na kukabiliana kwa risasi na washambuliaji waliokuwa na silaha ndani ya hoteli. Saa nne baadae, msemaji wa serikali Ismael Mukhtaar Omar alituma ujumbe kwenye ukurasa wa Tweeter akisema kuwa uvamizi huo umekwisha na wavamizi wote wameuawa.