MALI-AU-SIASA-USALAMA

AU yalitaka jeshi la Mali 'kumuachilia mara moja' rais Keita

Wanajeshi wa Mali wakiingia katika eneo la Uhuru huko Bamako baada ya kundi la wanajeshi waasi kumkamata rais IBK na Waziri Mkuu Agosti 18, 2020.
Wanajeshi wa Mali wakiingia katika eneo la Uhuru huko Bamako baada ya kundi la wanajeshi waasi kumkamata rais IBK na Waziri Mkuu Agosti 18, 2020. STRINGER / AFP

Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), Cyril Ramaphosa, rais wa Afrika Kusini, amelaani "jaribio la mapinduzi" nchini Mali na kulitaka jeshi "kumachiliwa mara moja" rais Ibrahim Boubacar Keïta aliyekamatwa Jumanne jioni na jeshi la nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyotolewa na rais wa Afrika Kusini, Bwana Ramaphosa "amelaani kitendo cha kubadili madaraka kinyume na katiba nchini Mali" na "amelitaka jeshi kumuachilia rais IBK, waziri mkuu na mawaziri wengine", na kutoa wito kwa jeshi "kurudi makambini”.

Wanajeshi walianza uasi huo mapema siku ya Jumanne katika mji wa Kati, uliopo kilometa 15 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Bamako ambapo milio ya risasi ilisikika. Taarifa za kukamatwa viongozi wa serikali zilipokelewa kwa furaha na umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katikati ya mji kwa ajili ya kushinikiza Keita kujizulu

Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Umoja wa Ulaya zote zimelaani uasi huo na kuonya juu ya jaribio lolote la kubadili madaraka kinyume na katiba katika taifa hilo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka "kuachiwa haraka na bila masharti" kwa rais Keita na Cisse wakati wanadiplomasia mjini New York wakisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura hii leo kwa ajili ya kujadili hali nchini Mali.

Wakati huo huo wanajeshi waliongoza mapinduzi nchini Mali na kupelekea kujiuzulu kwa rais Aboubakar Keita na serikali yake wamesema kuwa wanapanga kuunda serikali ya mpito ya kiraia itakayoandaa uchaguzi mpya.

Kupitia taarifa yao iliyorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha taifa , msemaji wa kundi la wanajeshi walioasi, Kanali Ismael Wague, amesema waliamua kuchukua uamuzi huo ili kuzuia nchi hiyo kutumbukia kwenye machafuko zaidi.

Kanali Ismael Wague ameyakaribisha makundi ya kiraia na vyama vya siasa kujiunga pamoja na kutayarisha muongozo wa kipindi cha mpito utakaowezesha kufanyika uchaguzi mkuu.