MALI-SIASA-USALAMA

Mali: Jamii ya kimataifa yalaani hatua ya jeshi

Ibrahim Boubacar Keïta, Juni 30, 2020.
Ibrahim Boubacar Keïta, Juni 30, 2020. AFP/Ludovic Marin

Hatua ya jeshi la Mali imeendelea kulaaniwa kote ulimwenguni, baada ya kuchukuwa madaraka kwa nguvu na kumshinikiza rais Ibrahim Boubakar Keita na waziri wake mkuu Boubou Cisse kujiuzulu usiku wa kuamkia leo Jumatano.

Matangazo ya kibiashara

"Mipaka yote ya nchi kavu na angani imefungwa hadi itakapochukuliwa hatua mpya," msemaji wa Kamati ya Kitaifa, ambayo imechukua madaraka ametangaza jana usiku kwenye runinga ya taifa ORTM. amebaini kuwa mikataba yote ya kimataifa itaheshimishwa na kwamba vikosi kama Minusma (kikosi cha umoja wa mataifa) au hata Barkhane, G5 Sahel na kikosi cha Takuba "wataendelea kubaki kuwa washirika wa Mali kwa kurejesha utulivu". "Mikataba yote iliyofikiwa", hasa mchakato wa Algiers uliosainiwa mwaka 2015, utaheshimishwa.

Wakati huo huo jamii ya kimataifa imeenbdelea kulaani jaribio hilo la mapinduzi nchini Mali.

Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika zote zimelaani uasi huo na kuonya juu ya jaribio lolote la kubadili madaraka kinyume na katiba katika taifa hilo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka "kuachiwa haraka na bila masharti" kwa rais Keita na Cisse wakati wanadiplomasia mjini New York wakisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura hii leo kwa ajili ya kujadili hali nchini Mali.

Kauli kama hiyo ya kutaka Keita kuachiwa pia imetolewa na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat. ECOWAS kwenye taarifa yake, imewataka wanajeshi kurejea kwenye kambi na kujizuia dhidi ya "kitendo chochote kinyume na katiba" na kujaribu kutatua tofauti za kisiasa kupitia mazungumzo.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umesema "unalaani jaribio la mapinduzi nchini Mali na unakataa mabadiliko yasiyo ya kikatiba".

Kumekuwa na hasira miongoni mwa wanajeshi ambao wanalalamikia kutolipwa mishahara yao lakini pia kuendeleka kuwepo kwa makundi ya kijihadi kulionekana kuwachosha wananchi.

Miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na maandamano yakiongozwa na wapinzani, chini ya Imam Mhmoud Dicko, wakitaka mageuzi ya kisiasa.

Keita, alichaguliwa rais wa Mali mwakka 2013 na kuchaguliwa tena kwa awamu nyingine ya miaka metano, lakini changmoto za utovu wa usalama na kisiasa, zimemwondoa madarakani.