MALI-SIASA-USALAMA

Mali: Wanajeshi walioasi kuunda serikali ya mpito na kutoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi

Wanajeshi waliofanya mapinduzi walihutubia taifa Jumatano hii, Agosti 19 asubuhi kwenye runinga ya taifa, ORTM.
Wanajeshi waliofanya mapinduzi walihutubia taifa Jumatano hii, Agosti 19 asubuhi kwenye runinga ya taifa, ORTM. AFP

Mapema Jumatano hii asubuhi, Agosti 19, wanajeshi walioasi wametoa wito wa kuundwa kwa serikali ya mpito ya kiraia na itakayowezesha kufanyika kwa uchaguzi.

Matangazo ya kibiashara

Wanajeshi hao pia wametangaza kuunda Kamati ya Kitaifa kwa niaba ya raia. Wanajeshi walio madarakani pia wamesema kwamba mikataba yote ya kimataifa itaheshimishwa.

"Sisi, vikosi vya uzalendo viliungana pamoja ndani ya Kamati ya Kitaifa kwa niaba ya raia (CNSP), tumeamua kuchukua majukumu yetu kwa kulinda raia", msemaji wa wanajeshi hao waasi, Kanali-Meja Ismaël Wagué, Naibu Mkuu wa jeshi la anga, amesema kwenye runinga ya taifa ORTM.

Askari hao, walioshika madaraka nchini Mali na kushinikiza Rais Ibrahim Boubacar Keïta kujiuzulu, wanasema wanataka kuunda "serikali ya mpito ya kiraia" ambayo itawezesha kufanyika kwa uchaguzi kwa "muda muafaka".

Katika hotuba yake, Ismaël Wagué pia amehakikisha kwamba mikataba yote ya kimataifa itaheshimishwa. Pia amebaini kwamba vikosi kama vile Minusma (kikosi cha umoja wa mataifa) au hata Barkhane, G5 Sahel na kikosi cha Takuba "wataendelea kubaki kuwa washirika wa Mali kwa kurejesha utulivu". "Mikataba yote iliyofikiwa", hasa mchakato wa Algiers uliosainiwa mwaka 2015, utaheshimishwa.

Wanajeshi walianza uasi huo mapema siku ya Jumanne katika mji wa Kati, uliopo kilometa 15 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Bamako ambapo milio ya risasi ilisikika.

Mapema siku ya Jumanne, serikali ya Mali ilitoa taarifa ya kutaka utulivu na kusema iko tayari kwa mazungumzo. Mali imekuwa ikijaribu kurejesha utulivu tangu maelfu ya wafuasi wa upinzani walipoingia barabarani wakimtuhumu Keita kwa ufisadi na kudhoofika kwa usalama katika eneo la kaskazini na kati pamoja na udanganyifu katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Aprili. Lakini kampeni dhidi ya

Keita iliongezeka mwezi uliopita baada ya watu 11 kuuwawa wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama, kufuatia maandamano ya siku tatu. Mazungumzo baina ya serikali na upinzani, yanayoongozwa na mhubiri maarufu Mahmoud Dicko, mshirika wa zamani wa Keita yaligonga mwamba.

Hatua hiyo ya jeshi imelaaniwa vikali na viongozi wa nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa pamoja na Ufaransa na kutaka wanajeshi kurejea kambini.