MALI-SIASA-USALAMA

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar aachia ngazi

Vikosi vya jeshi la Mali wakishangiliwa na umati wa watu kufuatia kukamatwa kwa Rais IBK na Waziri Mkuu Boubou Cissé Agosti 18, 2020.
Vikosi vya jeshi la Mali wakishangiliwa na umati wa watu kufuatia kukamatwa kwa Rais IBK na Waziri Mkuu Boubou Cissé Agosti 18, 2020. STRINGER / AFP

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ametangaza kujiuzulu  baada ya kukamatwa na kuzuiwa na wanajeshi siku ya Jumanne, hatua ambayo imezua hali ya sintofahamu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Akihotubia raia wa nchi hiyo, Keita ametangaza pia kulivunja bunge na serikali, huku akisema hataki damu yoyote imwagike kwa  sababu yake, iwapo ataendelea kuwa madarakani.

Hatua hii imekuja saa chache baada ya yeye na Waziri Mkuu Boubou Cisse kukamatwa na kuzuiwa katika kambi ya jeshi jijini Bamako.

Hatua hiyo ya jeshi imelaaniwa vikali na viongozi wa nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, Umoja wa Afrika,  Umoja wa Mataifa pamoja na Ufaransa na kutaka wanajeshi kurejea kambini.

Kumekuwa na hasira miongoni mwa wanajeshi ambao wanalalamikia kutolipwa mishahara yao lakini pia kuendeleka kuwepo kwa makundi ya kijihadi kulionekana kuwachosha wananchi.

Miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na maandamano yakiongozwa na wapinzani, chini ya Imam Mahmoud Dicko, wakitaka mageuzi ya kisiasa.

Keita, alichaguliwa kuwa rais wa Mali mwaka 2013 na kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka mitano, lakini changamoto za utovu wa usalama na kisiasa, zimemwondoa madarakani.