DRC-USALAMA-HAKI

DRC: Mtu mmoja akamatwa katika uchunguzi wa mauaji ya mbunge Nsukami

Mji wa Matadi, mji mkuu wa mkoa wa Kongo ya Kati, DRC (picha ya kumbukumbu).
Mji wa Matadi, mji mkuu wa mkoa wa Kongo ya Kati, DRC (picha ya kumbukumbu). MONUSCO/Myriam Asmani

Baada ya mauaji ya mbunge wa mkoa wa Kongo ya Kati, Albert Nsimba Nsukami, Agosti 15 katika mji wa Matadi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vyanzo kadhaa vimetangaza kukamatwa kwa mtuhumiwa ambaye, kulingana na watoto wa mbunge huyo, alikuwa katika kundi la washambuliaji.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya majibizano kati ya kundi hilo la washambuliaji na familia ya mbunge aliyeuawa, washambuliaji walitimka baada ya kutekeleza mauaji hayo na kusahau bunduki moja. Kwa mujibu wa vyanzo huko Matadi, katika jaribio la kutaka kupata bunduki hiyo, mtu mmoja asiyejulikana alijitokeza asubuhi katika nyumba ya mbunge Albert Nsimba Nsukami, baada ya mauaji hayo. Alijifananisha kama mkuu wa mkoa. Lakini mkuu rasmi wa mkoa, wakati huo, alikuwa katika chumba cha kuhifadhi maiti na familia ya marehemu kwa kuhifadhi mwili wake.

Bunduki yenyewe aina ya AK-47, ilikuwa tayari imechukuliwa na polisi ambao walikuwa wamewasili eneo la tukio muda mfupi baada ya mauaji hayo.

Uchunguzi ulifunguliwa mara moja. Mtuhumiwa, alirudi katika eneo la la tukio, na kutambuliwa na watoto wa mbunge aliyeuawa.

Watoto hao wamebaini kwamba mtu huyo ndiye yule aliyevutana na baba yao kabla ya kuuawa.

Sababu za mauaji hayo bado hazijajulikani kufikia sasa. Baadhi wanadai kuwa ni uhalifu tu wa kawaida, wengine wanasema ni mauaji ya kisiasa.