MALI-ECOWAS-SIASA-USALAMA

Mvutano waendelea kati ya ECOWAS na jeshi kuhusu raia kurejea kwenye utawala Mali

Ujumbe wa ECOWAS, ukiongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan.
Ujumbe wa ECOWAS, ukiongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan. ANNIE RISEMBERG / AFP

Mazungumzo kati ya wawakilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, na jeshi linaloshikilia madaraka nchini Mali, hadi leo hayajazaa matunda yoyote.

Matangazo ya kibiashara

Pande hizo mbili zilimaliza mazungumzo yao bila kufikia makubaliano yoyote kuhusu masharti ya kukabidhi madaraka kwa raia. Jeshi lilikuwa limetangaza kuunda serikali ya mpito kwa muda muafaka, wakati ECOWAS inataka taasisi zilizopinduliwa zirejeshwe mara moja.

Suala kuu la kutokubaliana kati ya kundi la jeshi linaloshikilia madaraka nchini Mali na timu ya usuluhishi ya ECOWAS linahusu muda wa kipindi cha mpito.

Awali, kundi la jeshi linaloshikilia madaraka, kama hoja ya msingi ya mazungumzo, lilipendekeza miaka mitatu, na Jumatatu wiki hii ilipendekeza miaka miwili ya kipindi cha mpito. Timu ya upatanishi kwa upande wake, kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger ambaye alishiriki mazungumzo hayo, inataka kipindi cha mpito kiwe kati ya miezi saba hadi kumi na mbili.

"Tayari wamependekeza miaka mbili leo asubuhi. Tunaona kuwa kipindi hiki ni kirefu. […] Tunachukulia kuwa ni hatua iliyopigwa lakini tunawaambia wafanye juhudi zaidi na hawajakataa. Wanasema wataifikiria zaidi, " amesema Kalla Ankouraou, Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger.

Kuhusu suala la rais wa mpito, ECOWAS inataka raia au mwanajeshi mtaafu ndiye achukuwe nafasi hiyo, lakini kundi la jeshi lililofanya mapinduzi, limefutilia mbali pendekezo hilo.