DRC-MAUAJI-USALAMA

Watu 20 wauawa katika shambulio la wapiganaji wa Kiislam Mashariki mwa DRC

Askari wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) wakiwa vitani huko Matombo, kilomita 35 kaskazini mwa Beni, Kaskazini Kivu, Januari 13, 2018.
Askari wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) wakiwa vitani huko Matombo, kilomita 35 kaskazini mwa Beni, Kaskazini Kivu, Januari 13, 2018. AFP

Wapiganaji wa kundi la waasi wa Kiislamu kutoka Uganda la ADF wanashtumiwa kuua watu wasiopungua 20 katika shambulio waliotekeleza katika vijiji vitatu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kilomita 30 kaskazini magharibi mwa mji wa Beni.

Matangazo ya kibiashara

Vyanzo kadhaa kutoka DRC, ikiwa ni pamoja na msemaji wa jeshi la FARDC na mwakilishi wa viongozi wa eneo hilo wamethibitisha taarifa hiyo baada ya kugunduliwa miili ya wahanga.

"Raia wamekata tamaa wakihofia usalama wao na wengine wamelazimika kuyatoroka makazi yao," amesema Rosette Kabula, naibu mkuu wa wilaya ya Beni, huku akiongeza "ni wakati wa kuomboleza."

Mauaji hayo yanatokea siku tatu baada ya shambulio kama hilo lililogharimu maisha ya watu 13katika vijiji vinavyopatikana kilomita 10 mashariki mwa mji wa Oicha.

"Jukumu letu kubwa ni kulinda nchi, lakini kwa bahati mbaya adui anatumia ujanja kwa kukwepa ngome zetu na kufanya mashambulizi dhidi ya raia wasi kuwa na hatia," msemaji wa jeshi la FARDC, Antony Mwalushayi amesema.

Wapiganaji wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi la wapiganaji wa Kiislam kutoka Uganda ambalo lmekita mizizi Mashariki mwa DRC kwa zaidi ya miaka 30, limeuwa raia zaidi ya 1,300 tangu mwanzoni mwa mwaka wa 2019, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.