MISRI-MUSLIM BROTHERHOOD-USALAMA-HAKI

Kiongozi Mkuu wa Muslim Brotherhood, Mahmoud Ezzat, akamatwa Cairo

Mahmoud Ezzat, mwaka 2005.
Mahmoud Ezzat, mwaka 2005. AFP PHOTO/KHALED DESOUKI

Kiongozi Mkuu wa Muslim Brotherhood Mahmoud Ezzat, 76, anazuiliwa jela tangu mapema leo Ijumaa (Agosti 28) katika kitongoji chenye makazi jijini Cairo, wizara ya mambo ya ndani ya Misri imesema.

Matangazo ya kibiashara

Mahmoud Ezzat alikuwa anatafutwa kwa miaka saba, na wengi walikuwa wameamini kuwa alifanikiwa kuondoka Misri na kukimbilia nchini Uturuki au Qatar. Hata hivyo, amekamatwa leo Ijumaa karibu na makao makuu ya Wizara ya Mambo ya ndani.

Agosti 30, 2013, Mohamad Baddie, kiongozi mkuu wa nane wa Muslim Brotherhood alikamatwa, siku chache baadae naibu wake Mahmoud Ezzat alitangazwa kuwa kiongozi wa kundi hilo nchini Misri na nje ya nchi.

Kulingana na makubaliano ya kundi la Muslim Brotherhood, kiongozi mkuu anapokamatwa, majukumu yake huchukuliwa moja kwa moja na naibu wake.

Vyanzo vilivyo karibu na Wizara ya Mambo ya ndani vinasema Mahmoud Ezzat alikimbilia Gaza kabla ya kurudi nchini Misri ili kuongoza vizuri kundi la Muslim Brotherhood.

Mahmoud Ezzat ni mwanafunzi wa Sayed Qotb, mtu mwenye nadharia ya kuchukuwa madaraka kwa kutumia nguvu ya kijihadi. Alihukumiwa adhabu ya kifo mara mbili kwa kosa la kushirikiana na nchi za kigeni kwa kudukuwa siri za nchi, na mashambulizi kadhaa ya kigaidi.

Wataalam katika idara ya polisi hivi sasa wanachunguza komputa na simu za kiongozi huyo aliyekamatwa kwa habari zaidi zitakazowezesha kuliangamiza kundi hilo la Muslim Brotherhood.