DRC-UN-MUKWEGE-UCHUNGUZI-HAKI

DRC: Umoja wa Mataifa walaani vitisho vya kuuawa dhidi ya Dkt Mukwege

Denis Mukwege akilakiwa na umati wa watu huko Bukavu, Desemba 27, 2018.
Denis Mukwege akilakiwa na umati wa watu huko Bukavu, Desemba 27, 2018. Fredrik Lerneryd / AFP

Tangu kupokea tuzo yake, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake anayejitolea kutibu wanawake waliokumbwa na ubakaji na ukatili wa kingono nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anaendelea kukemea ukatili unaoendelea kutekelezwa nchini humo na kuomba haki kwa uhalifu uliofanywa wakati wa vita.

Matangazo ya kibiashara

Katika wiki za hivi karibuni, yeye na familia yake wamekuwa wakipata vitisho vya kuuawa. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani vitisho hivi kwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet imesema maisha ya Dr Mukwege yamo katika hatari kubwa na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi usiopendelea upande wowote kuhusiana na vitisho hivyo.

Tuna wasiwasi sana kwa sababu tunaohofia maisha yake. Hasa kwa kuwa sio mara ya kwanza kufanyowa vitisho. Mwaka 2012 Mukwege alinusurika jaribio la mauaji, amesema Marta Hurtado, mmoja wa wasemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na Sonia Rolley

Itakumbuka kwamba, wakati wa kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Mawaziri, siku nane zilizopita, Rais Tshisekedi aliitaka serikali kumlindia usalama Daktari Mukwege na kuagiza kuanzishwa kwa uchunguzi.

Mukwege alipewa Tuzo la Amani la Nobel mwaka 2018 kwa kazi yake nzuri kama daktari wa wanawake na uzalishaji katika Hospitali ya Panzi ambayo hupokea maelfu ya wanawake kila mwaka, wengi wao wakihitaji upasuaji kutoka kwa unyanyasaji wa kingono.

Hospitali hiyo iko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, eneo ambalo limegubikwa na vurugu za kikabila na hujuma za wanamgambo na makundi mbalimbali ya waasi, na vilevile operesheni za jeshi la taifa.