LIBYA-SIASA-USALAMA

Libya: Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya umoja wa kitaifa asimamishwa kazi

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya Fathi Bashagha, kutoka serikali ya umoja wa kitaifa, amesimamishwa kazi Agosti 28, 2020.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya Fathi Bashagha, kutoka serikali ya umoja wa kitaifa, amesimamishwa kazi Agosti 28, 2020. Mahmud TURKIA / AFP

Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya umoja wa kitaifa, Fathi Bashagha, amefutwa kazi. Kusimamishwa kwake kunahusiana na maandamano ya siku za hivi karibuni ambayo yalizimwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na taarifa kutoka serikali ya umoja wa kitaifa, Waziri wa Mambo ya Ndani "amesimamishwa kazi kwa muda". Atajibu "uchunguzi wa kiutawala" juu ya "taarifa zake kuhusu maandamano na matukio" yaliyotokea Tripoli.

Tangu Jumapili maandamano kadhaa yamefanyika katika mji mkuu dhidi ya ufisadi na kuzorota kwa hali ya maisha. Matukio mabaya yalishuhudiwa. Siku ya Jumapili watu wenye silaha walifyatua risasi za moto kutawanya umati wa waandamanaji, na kujeruhi watu kadhaa.

Waziri wa mambo ya ndani ametupilia mbali kuhusika kwake katika ukandamizaji huo na kushutumu makundi yenye silaha yasiyojulikana kuwateka nyara na kuwazuia waandamanaji aliowaita "wa amani".

Kusimamishwa kwake kunakuja wakati kukiwa na uhasama kati ya waziri mkuu na waziri wake wa mambo ya ndani. Fayez el-Sarraj, akiungwa mkono na wanamgambo kutoka Tripoli, anazidi kugombewa. Na Fathi Bashagha, akiungwa mkono na Ankara na wanamgambo wa Misrata, ana nia ya kuchukua uongozi wa serikali ya Tripoli.

Naibu Katibu kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani Khaled Tijani Mazen ameteuliwa kukaimu nafasi hiyo kwa kusubiri uamuzi.