DRC-HAKI

Denis Mukwege alalamika dhidi ya ukosefu wa haki kwa uhalifu nchini DRC

Denis Mukwege kwenye mkutano na waandishi wa habari huko Tokyo, Oktoba 3, 2019.
Denis Mukwege kwenye mkutano na waandishi wa habari huko Tokyo, Oktoba 3, 2019. Behrouz MEHRI / AFP

Licha ya vitisho vya kuuawa, Dkt Denis Mukwege anaendelea na juhudi zake na amesema hatavunjika moyo. Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ameonekana kwa mkutano wa video kutoka Bukavu wakati wa kikao cha kamati ya haki za binadamu cha Bunge la Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Mukwege amesema bila kuhukumu uhalifu wa zamani, ukiukaji wa haki za binadamu utaendelea kuongezeka nchini mwake.

Mbali na kufanyiwa vitisho, Dkt Mukwege ameendelea kusema akisisitiza juu ya kkuzorota kwa hali ya haki za binadamu nchini mwake. Ametaja takwimu za ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka. "Kwa wastani, raia wanane wanauawa kila siku katika machafuko yanayoendelea. Idadi hiyo ni kubwa. Na mara nyingi, wanawake na watoto ndio waathirika wakuu. Siku baada ya siku, mwezi baada ya mwezi, mwaka baada ya mwaka, ukiukaji mpya wa haki za binadamu unashuhudiwa, unatathiminiwa na unaripotiwa, " amesema Dkt Mukwege.

Kwa mujibu wa Dkt Mukwege, ni kwa sababu wauaji wa waliohusika na uhalifu uliopita bado wamejificha ndani ya majeshi na taasisi za DRC na nchi za eneo hili ambapo ukiukwaji huu unaendelea.

Ameomba kuundwa kwa mahakama ya kimataifa ya jinai ambayo itaweza kushughulikia uhalifu wa kivita, lakini pia iwe na mamlaka ya kuhukumu uhalifu uliyotokea miaka ya nyuma hadi leo.

"Kukosekana kwa utashi wa kisiasa na sera ya kweli kwa muda mrefu ndio inasababisha kukosekana kwa haki na ukweli. Hali hii ndio inasababisha mauaji yanaendelea. Hali hii ambayo inatia aibu dhamira yetu ya pamoja ya ubinadamu haiwezi kudumu tena, " ameongeza Dkt Mukwege.

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel amekaribisha mpango wa rais Tshisekedi - "mwanasiasa asiyehusiana na uhalifu wa zamani, ambaye anataka nchini DRC kuanzishwe utaratibu wa kuundwa kwa mahakama itakayoshuhugulikia uhalifu wa kivita, " amebaini Dkt Mukwege.

Lakini mwanzoni mwa mwezi Agosti, rais Tshisekedi alilaumu juu ya ukosefu wa maendeleo kwenye mpango huo unaojadiliwa katika ngazi ya serikali.