DRC-USALAMA

DRC: Kundi la waasi wa Codeco lawateka nyara watu zaidi ya 40 Ituri

Wilaya ya Aru, katika Mkoa wa Ituri, DRC: Jua linazama kwenye Mto Aru, Wilaya ya Aru, Mkoa wa Ituri.
Wilaya ya Aru, katika Mkoa wa Ituri, DRC: Jua linazama kwenye Mto Aru, Wilaya ya Aru, Mkoa wa Ituri. Monusco/Anne Herrmann

Takriban watu 42 wanaendelea kushikiliwa mateka na kundi la waasi wa Codeco. Waru hao walitekwa nyara Alhamisi wiki iliyopita katika kijiji cha Shaba katika eneo la Aru, katika mkoa wa Ituri, Mashariki mwa DRC.

Matangazo ya kibiashara

Watu hawa walitekwa nyara kufuatia shambulio lililodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Codeco.Shambulio hilo lililolenga mji huo wa madini liligharimu maisha ya watu wasiopungua watatu kulingana na mamlaka kutoka eneo hilo. Hali hiyo imeongeza wasiwasi zaidi kwani eneo hili lilikuwa halijakumbwa na machafuko yanayosababishwa na watu wenye silaha.

Wakiwa walijihami na visu na silaha za moto, wauaji hao walitumia fursa hiyo ya usiku kuingia katika jiji hilo linalokaliwa na wafanyabiashara wa madini. Mkuu wa machimbo hayo na watu wengine wawili waliuawa papo hapo. Walizikwa siku ya Jumapili. Eneo hilo linalopatikana karibu kilomita mia moja kutoka mji wa Aru, mji mkuu wa jimbo la Aru, lilishuhudia visa vya uporaji.

Kulingana na vyanzo kutoka eneo hilo, baadhi ya watu waliotekwa nyara walitumiwa kusafirisha mali iliyoporwa.

Kufikia sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu waliko watu hao.

Mkuu wa Wilaya ya Aru anatarajia kuondoka leo mji huo na kuelekea katika eneo la shambulio.

Wakati huo huo, viongozi wa zamani wa kivita waliotumwa na Felix Tshisekedi kujaribu kushinikiza makundi yenye silaha kuweka chini silaha bado wamekwama huko Ituri. Sasa wanalenga mikoa ya madini. Wiki mbili zijazo, watakuwa karibu kilomita 35 kutoka Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri. Kutoka hapo, wameaahidi kuanzisha majadiliano, ili waweze kupata habari zaidi kuhusu shambulio la siku ya Alhamisi.

Gavana wa jimbo hilo bado yuko Kinshasa. Siku ya Jumatatu, alishiriki katika mkutano wa dharura ulioongozwa na rais Félix Tshisekedi. Mkutano huo ulizungumzia hasa kuhusu sualama la usalama na maendeleo kuhusu eneo la mashariki mwa nchi.