AFRIKA KUSINI-AFYA

Afrika Kusini: Wahudumu wa afya waandamana dhidi ya mazingira yao za kazi

Waandamanaji wakiitikia wito wa chama cha wafanyakazi katika sekta ya umma Afrika Kusini NEHAWU huko Pretoria, Septemba 3, 2020
Waandamanaji wakiitikia wito wa chama cha wafanyakazi katika sekta ya umma Afrika Kusini NEHAWU huko Pretoria, Septemba 3, 2020 REUTERS/Siphiwe Sibeko

Wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Afrika Kusini wameendelea kupinga mazingira yao ya kazi, huku wakiitikia wito wa chama cha wafanyakazi katika sekta ya umma, NEHAWU.

Matangazo ya kibiashara

Karibu watu 100 walikusanyika Alhamisi wiki hii nje ya majengo ya ikulu ya rais huko Pretoria kudai mazingira bora ya kazi na nyongeza ya mshahara.

Wanasikitishwa kuona serikali haizingatii zaidi mahitaji yao, licha ya kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliana na janga la Corona katika nchi ambayo imeathirika vibaya na ugonjwa.

Mokgope Frans, muuguzi wa sekta ya umma na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wa NEHAWU ni miongoni mwa waandamanaji, amesema kuwa ameghadhabishwa na kuona kwamba serikali haijarejelea uamuzi wake wa kusimamisha mishahara ya wafanyakazi.

“Sisi wafanyakazi tumechoka, hali sasa imekithiri. Kufikia sasa, hatujapokea nyongeza yoyote au marupurupu yoyote, ingawa juhudi nyingi zimefanywa. Makubaliano ya kuongeza mshahara lazima yatekelezwe haraka iwezekanavyo, " Mokgope Frans amesema.

Zaidi ya wafanyakazi 27,000 katika sekta afya nchini Afrika Kusini wameambukizwa virusi vya Corona, na 240 wamefariki dunia.

Kwa wale wanaoendelea kufanya kazi, kama Irene Mothibe, mara nyingi wanakabiliwa na ukosefu wa wafanyakazi. “Wauguzi wanaopata virusi vya Corona wanalazimika kubaki nyumbani, kwa hivyo idadi ya wafanyakazi inapungua, na kazi zinaongezeka wakati malipo yanasalia pale pale. Sisi ni 'wafanyikazi muhimu' tu kwenye karatasi, linapokuja suala la kulipa wauguzi, linakuwa ni jambo lingine, " Irene Mothibe amesema.