DRC-HAKI

DRC: Christian Ngoy Kenga Kenga, aliyehusika katika kesi ya Chebeya, akamatwa

Christian Ngoyi anashtumiwa kuhusika katika mauaji ya Floribert Chebeya na Fidèle Bazana mwaka 2010 (picha ya kumbukumbu)
Christian Ngoyi anashtumiwa kuhusika katika mauaji ya Floribert Chebeya na Fidèle Bazana mwaka 2010 (picha ya kumbukumbu) AFP PHOTO / JUNIOR D. KANNAH

Christian Ngoy Kenga Kenga, kamanda wa bataliani ya Simba, nchini DRC, aliyehusika katika mauaji ya Floribert Chebeya na Fidèle Bazana, mwaka 2010 amekamatwa.

Matangazo ya kibiashara

Afisa huyo wa polisi aliyechukuliwa kama mtoro, kutokana na makosa mbalimbali aliyotekeleza, anatuhumiwa kumiliki silaha za kivita.

Mazingira ya kukamatwa kwa Christian Ngoyi Kenga Kenga bado hayajafahamika.

Vyanzo kutoka idara ya ujasusi vinabaini kwamba Christian Ngoyi Kenga Kenga alikamatwa mjini Lubumbashi na kusafirishwa mjini Kinshasa baada ya kupatikiana na hatia ya kumiliki silaha za vita. Afisa huyo wa jeshi kabla ya kuhamishiwa katika idara ya polisi, anatajwa katika visa kadhaa vya uhalifu.

Tukio baya na ambalo halitosahaulika miongoni mwa maovu aliyotenda ni ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa kundi la Bundu dia Kongo mwaka 2008 katika mkoa wa Kongo ya Kati (Kongo Central), na mauaji ya mwanaharakati wa shirika la kutetea haki za binadamu la "la Voix des Sans Voix" Floribert Chebeya na Fidèle Bazana mwaka 2010.

Kwa kutoroka haki, mtu huyo, baada ya kupewa msaada na washirika wake, aliondolewa katika mji wa Kinshasa, na kuhamishiwa kikazi mjini Lubumbashi. Wakati huo Christian Ngoyi aliongezewa cheo kutoka Meja hadi Kanali.

Mtu mwingine aliyetajwa katika kesi hiyo ya mauaji ya Floribert Chebeya na dereva wake Fidèle Bazana ni Paul Mwilambwe, ambaye alikimbilia Ubelgiji baada ya kupitia nchini Senegal. Tayari alijisalimisha kwa haki na anaomba kupelekwa nchini DRC ili kusema ukweli wote juu ya mauaji ya watetezi hao wawili wa haki za binadamu kwenye makao makuu ya Polisi.

Paul Mwilambwe anasema aliona mwenyewe kwa macho yake tukio hilo na anamshtumu Christian Ngoyi na Jenerali John Numbi kuhusna na mauaji hayo.