LIBYA-UN-WAHAMIAJI-USALAMA

Antonio Guterres ataka kufungwa kwa vituo wanakozuiliwa wahamiaji nchini Libya

Karibu wahamiaji 3,000 wanaaminika kuwa ni wafungwa nchini Libya (picha ya kumbukumbu)
Karibu wahamiaji 3,000 wanaaminika kuwa ni wafungwa nchini Libya (picha ya kumbukumbu) Taha JAWASHI / AFP

Umoja wa Mataifa unatiwa wasiwasi na hali ambayo raia wa Libya wanaishi na hasa wahamiaji ambao wanajikuta wamekwama nchini humo. Wahamiaji hao wanakwama katika nchi ambayo inaendelea kukumbwa na mgogoro wa kivita kati ya serikali ya umoja wa kitaifa na Jeshi la Ukombozi wa kitaifa la Jenerali Khalifa Haftar. 

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatoa wito wa kufungwa kwa vituo wanakozuiliwa wahamiaji haramu, na amepinga dhidi ya ukiukaji wa haki zao.

Hatima ya wananchi wa Libya, na hasa wahamiaji, imeendelea kuzua wasiwasi mkubwa kwa upande wa Umoja wa Mataifa katika miezi ya hivi karibuni. Ripoti hii ya Antonio Guterres inaonyesha wazi dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kulinda raia, licha ya kuendelea kwa mgogoro nchini Libya.

Katibu Mkuu anazungumza juu ya "hali mbaya" ya kuwekwa kizuizini kwa watu 2,780: ukosefu wa huduma za kiafya au chakula, mateso, visa vya watu kutoweka, unyanyasaji wa kijinsia ... Wahamiaji hawa waliokusanywa katika vituo tofauti wanaendelea kukumbwa na madhila mbalimbali. Kwa muda mwingi wanatumiwa kufanya kazi ya bila malipo ususan kukarabati au kuosha silaha za makundi yenye silaha, vijana (wavulana na wasichana) pia hudhalilishwa.

Karibu robo ya wafungwa hawa ni watoto, ambao kawaida hutenganishwa na familia zao - kinyume na kanuni zote za kimataifa, na Antonio Guterres anatoa wito kwa mamlaka nchini Libya kuwaachilia mara moja na kuwapa huduma maalum.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesikitishwa kwamba hakuna hatua yoyote iliyopigwa katika uchunguzi wa mashambulizi ya anga dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Tajoura, karibu na mji wa Tripoli, Julai 2019 - ambayo yaligharimu maisha ya watu zaidi ya 50.