MALI-IBK-AFYA-SIASA

Rais wa zamani wa Mali apelekwa katika Umoja wa Falme za Kirabu kwa matibabu

Ibrahim Boubacar Keïta, Juni 30, 2020.
Ibrahim Boubacar Keïta, Juni 30, 2020. AFP/Ludovic Marin

Rais wa zamani wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta aliondoka jijini Bamako Jumamosi jioni Septemba 5 kuelekea katika Umoja wa Falme za Kiarabu kwa matibabu, kulingana na vyanzo vya uwanja wa ndege.

Matangazo ya kibiashara

Kuondoka kwa Ibrahim Boubacar Keïta (IBK) kulitarajiwa kwa siku kadhaa kwa sababu ya hali yake ya kiafya.

Afya ya kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 75 imekuwa sio nzuri na kusababisha kulazwa hospitalini mara alipoachiwa baada ya kuzuiliwa na watawala wa kijeshi kwa siku 10.

Jumamosi hii, Septemba 5 asubuhi, ndege maalum ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji mkuu Bamako, kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kwa siku kadhaa, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali walikuwa katika mazungumzo ya kumsafirisha Ibrahim Boubacar Keïta, kwa ajili ya matibabu kutokana na hali yake ya afya. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali pia uliunga mkono mchakato huo.

Hapo awali, kulingana na makubaliano kati ya kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi na ECOWAS, rais wa zamani aliyetimuliwa mamlakani alitarajiwa kukaa mwezi mmoja huko Bamako kabla ya kufikiria kwenda nje kwa matibabu. Lakini wakati huo huo, rais wa zamani alilazwa katika kliniki ya Pasteur katika mji mkuu.

Wakati huo wawakilishi wa ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika walikutana na kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini humo na kukubaliana kumruhusu IBK kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo pande hizo zilikubaliana kwamba ikiwa vyombo vya sheria vya Mali vitamhitaji IBK, atakuwa mwepesi wa kuripoti.

Kiongozi huyo wa Mali aliyeondolewa madarakani ameandamana na mkewe, Aminata Maiga Keita, msaidizi, madaktari wawili na maafisa wanne wa usalama, hayo ni kwa mujibu wa Mamadou Camara mkuu wa zamani wa wafanyakazi wa Boubacar Keita aliyeliambia shirika la habari la Reuters kuwa Keita aliondoka kutoka mjini Bamako Jumamosi jioni ndani ya ndege iliyokodishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu kufuatia ombi kutoka kwa mamlaka ya Mali na Keita mwenyewe, ili aweze kwenda kutibiwa katika hospitali ya kijeshi katika mji wa Abu Dhabi.

Camara amesema hiyo ni ziara ya matibabu itakayochukua muda wa kati ya siku 10 hadi 15.