COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA

Côte d'Ivoire: Upinzani waendelea kulalamika dhidi ya hatua ya Alassane Ouattara kuwaia muhula mwingine

Rufaa kadhaa zimewasilishwa kwa Baraza la Katiba kujaribu kubatilisha uchaguzi wa rais anayemaliza muda wake.
Rufaa kadhaa zimewasilishwa kwa Baraza la Katiba kujaribu kubatilisha uchaguzi wa rais anayemaliza muda wake. SIA KAMBOU / AFP

Wagombea kadhaa wa upinzani waliotangazwa hivi karibuni nchini Côte d'Ivoire wamewasilisha rufaa kwa Mahakama ya Katiba, ambayo inatarajia kuidhinisha wagombea katika kinyang'anyiro cha urais nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Wagombea wa upinzani wanataka Mahakama ya Katiba imtangaze Alassane Ouattara kwamba hana vigezo vya kushiriki katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 31.

Kulingana na Katiba ya Côte d'Ivoire rais anatakiwa kuhudumu kwa mihula miwili pekee ikiwa rais atabahatika kuchaguliwa kwa muhula wa pili.

Lakini kulingana na kambi ya rais, kupitishwa kwa sheria mpya ya msingi mwaka 2016 kumefanya mambo yote yabadilike.

Tangu kutangazwa orodha ya muda ya wagombea urais 44 wiki iliyopita, kipindi cha kukata rufaa kimefunguliwa.

Machi 5 rais Emmanuel Macron alikaribisha tangazo la Alassane Ouattara la kutowania muhula mwingine, akimwita "mtu mwenye busara na kiongozi wa serikali mwenye hekima".

Lakini, tangu rais wa Côte d’Ivoire kubadili kauli, Agosti 6, na kutangaza kuwa yuko tayari kuwania katika uchaguzi wa urais ujao, Paris imekaa kimya.Kwa hiyo upinzani nchini Côte d’Ivoire umiomba Paris kuonyesha msimamo wake.

Hivi karibuni Pascal Affi N’Guessan, ambaye ni mgombea wa chama cha upinzani cha FPI alimwandikia rais wa Ufaransa barua ya wazi akibaini kwamba tangazo la Alassane Ouattara kuwania muhula mwingine, ni "mapinduzi ya taasisi", na ni "chanzo cha mgogoro". "Alassane Ouattara anakuja kukuomba uungwaji wako mkono kwa uhalifu wake, tunataka angalau uonyeshe msimamo wako kufuatia uamuzi wake," Pascal Affi N’Guessan aliandika. "Ukimya wako (…) unatafsiriwa tofauti katika nchi yangu. Kauli yako inasubiriwa kwa hamu hapa nchini", aliongeza Waziri Mkuu wa zamani wa Côte d’Ivoire.

Na Spika wa zamanai wa nchi hiyo Guillaume Soro alimuandika barua rais wa Ufaransa akimtaka kuonysha msimamo wake kufuatia uamuzi wa Alassane Ouattara kutaka kuwania muhula mwingine.

Hata hivyo mawaziri mbalimbali wa serikali ya Côte d’Ivoire wamekuwa wakionyesha kwenye vyombo mbalimbali vya Ufaransa kuwa hatua ya Alassane Ouattara sio kinyume na katiba ya nchi.