AFRIKA-MAJANGA ASILI

Karibu watu 760,000 waathiriwa na mafuriko katika eneo la Sahel

Katika eneo la Keur Massar, karibu na mji wa Dakar, Septemba 8, 2020.
Katika eneo la Keur Massar, karibu na mji wa Dakar, Septemba 8, 2020. REUTERS/Zohra Bensemra

Kulingana na Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, karibu watu 760,000 wameathiriwa na mafuriko ambayo yameshambulia nchi kadhaa za Afrika Magharibi na sehemu za Afrika ya Kati kwa wiki kadhaa.

Matangazo ya kibiashara

Mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana zilisababisha mafuriko makubwa, na kuathiri zaidi ya watu milioni moja katika nchi kumi na moja.

Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA inasema ina wasiwasi kuwa takwimu hii inaweza kuzidi mwaka huu kwa sababu msimu wa mvua haujaisha.

Mji wa Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso unakumbwa na mafuriko kwa muda wa wiki moja. Serikali ya Burkina Faso, imebaini kwamba watu kumi na tatu wamepoteza maisha na hivyo kutangaza hali ya janga la asili jana Jumatano.

Nchini Ghana, pia, mvua kubwa na kuongezeka kwa kiwango cha maji vimeua watu kadhaa kaskazini mwa nchi.

Hali kama hiyo nchini Nigeria ambapo majimbo ya kaskazini ndiyo yameathirika zaidi. Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA imeripoti watu 30 waliopoteza maisha, jimbo la Borno pekee limeripoti watu 26,000 ambao hawana makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.

Hali ya kutisha nchini Sudan

Lakini Niger ndio imeathirika zaidi kutokana na mafuriko haya katika eneo hilo dogo lenye watu 330,000 walioathirika, 65 wamepoteza maisha na nyumba 34,000 zimeharibiwa, kulingana na takwimu zilizotolewa Jumatano na Waziri wa Haki za Kibinadamu wa Niger na uratibu wa majanga. Katika eneo la Mashariki, Chad na Cameroon pia zinakabiliwa na kuongezeka kwa viwango vya maji baharini, lakini hali ni ya kutisha zaidi nchini Sudan. Waziri wa Mambo ya nje wa Sudan anakadiria kuwa watu 500,000 wanaweza kuathiriwa moja kwa moja na mafuriko hayo ambayo yamesababisha vifo vya watu 101.Hali ya hatari ilitangazwa Ijumaa kwa miezi mitatu kote nchini.