DRC-UN-MUKWEGE-USALAMA

Umoja wa Mataifa kumpa ulinzi Daktari Denis Mukwege

Dk Denis Mukwege hapa katika Hospitali ya Panzi Machi, 18, 2015.
Dk Denis Mukwege hapa katika Hospitali ya Panzi Machi, 18, 2015. Marc JOURDIER / AFP

Umoja wa Mataifa umetangaza kumpa ulinzi mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Daktari Denis Mukwege, raia wa DRC, kufuatia vitisho vya mauaji dhidi yake baada yake kutaka haki kufanyika dhidi ya wanaokiuka haki za binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Umoja huo umesema maisha ya Daktari Mukwege yako hatarini baada ya yeye na familia yake kupokea vitisho kupitia simu yake ya mkononi  na mitandao ya kijamii.

Licha ya vitisho vya kuuawa, Dkt Denis Mukwege anaendelea na juhudi zake na amesema hatavunjika moyo. Hivi karibuni mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alionekana kwa mkutano wa video kutoka Bukavu wakati wa kikao cha kamati ya haki za binadamu cha Bunge la Ulaya.

Mbali na kufanyiwa vitisho, Dkt Mukwege ameendelea kusema akisisitiza juu ya kuzorota kwa hali ya haki za binadamu nchini mwake. Wiki jana alitaja takwimu za ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka. "Kwa wastani, raia wanane wanauawa kila siku katika machafuko yanayoendelea. Idadi hiyo ni kubwa. Na mara nyingi, wanawake na watoto ndio waathirika wakuu. Siku baada ya siku, mwezi baada ya mwezi, mwaka baada ya mwaka, ukiukaji mpya wa haki za binadamu unashuhudiwa, unatathiminiwa na unaripotiwa, " alisema Dkt Mukwege.

Kwa mujibu wa Dkt Mukwege, ni kwa sababu wauaji waliohusika na uhalifu uliopita bado wamejificha ndani ya majeshi na taasisi za DRC na nchi za eneo hili ambapo ukiukwaji huu unaendelea.

Aliomba kuundwa kwa mahakama ya kimataifa ya jinai ambayo itaweza kushughulikia uhalifu wa kivita, lakini pia iwe na mamlaka ya kuhukumu uhalifu uliyotokea miaka ya nyuma hadi leo.