DRC-AFRIKA YA KATI-USALAMA

Mkutano wa viongozi watano wa nchi za Afrika ya Kati waahirishwa

Mji mkuu wa DRC, ambako kulitarajiwa kufanyika mkutano wa viongozi watano wa nchi za Afrika ya Kati, mkutano ambao umeahirishwa kwa tarehe isiyojulikana.
Mji mkuu wa DRC, ambako kulitarajiwa kufanyika mkutano wa viongozi watano wa nchi za Afrika ya Kati, mkutano ambao umeahirishwa kwa tarehe isiyojulikana. Photo by Ute Grabowsky/Photothek via Getty Images

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetangaza kuahirishwa kwa kikao cha viongozi watano wa nchi za Afrika ya Kati, uliokuwa umepangwa kufanyika mjini Goma wiki ijayo, kujadiliana kuhusu hali ya usalama katika eneo la Maziwa Makuu.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya nje Marie Tumba Nzeza, akitoa tangazo hilo, amesema kuwa mkutano huo utafanyika tarehe nyingine.

Nzeza ameeleza kuwa, hatua ya kuahrishwa kwa mkutano huo umetokana na kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaoanza siku ya Jumanne jijini New York nchini Marekani na viongozi hao wanajiandaa kuhotubia mkutano huo.

Hata hivyo, kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Burundi ilikuwa imesema kuwa haitashiriki katika mkutano huo ambao ungewaleta viongozi kutoka Uganda, Rwanda, Angola pamoja na wenyeji Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Duru nyingine zinasema huenda sababu ya kuahirishwa kwa kikao hicho ni vibngozi wa Uganda kupendekeza kuwa, kifanyike mjini Lubumbashi ili kumwepusha rais Yoweri Museveni kupitia katika anga la Rwanda.

Uganda na Rwanda, katika miezi ya hivi karibuni, zimeendelea kuvutana na kusababisha uhusiano baridi kati ya nchi hizo jirani, na DRC pamoja na Angola zimekuwa zikijaribu kutatua mvutano huo.

Mbali na masuala ya usalama, viongozi wa nchi hizo walikuwa wamepanga pia kujadiliana kuhusu uhusiano wa kidiplomasia wa nchi zao na kuanza kurejesha ushirikiano wa kibiashara katika kipindi hiki cha janga la Corona.