BURKINA FASO-MAJANGA YA ASILI

Mafuriko katika Sahel: Misaada ya dharura yapelekwa kwa watu walioathirika zaidi

Moja ya maeneo ya mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, mwaka 2012.
Moja ya maeneo ya mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, mwaka 2012. REUTERS/Joe Penney/Files

Karibu raia 71,000 wa Burkina Faso wameathiriwa na mafuriko kulingana na takwimu rasmi. Mafuriko haya yalisababisha vifo vya watu 13 na 50 kujeruhiwa. Mamia ya familia sasa hawana makazi. Mahitaji ya haraka yanakadiriwa zaidi ya Faranga za CFA Bilioni 9.

Matangazo ya kibiashara

Mvua kubwa na upepo vimeharibu zaidi ya nyumba 5,000. Kulingana na takwimu rasmi karibu watu 71,000 wameathiriwa na mafuriko nchini Burkina Faso. Mamia ya watu wameachwa bila makazi. Wamepewa hifadhi kwa muda katika shule na vituo vya mapokezi. Karibu makazi 1,700 yameharibiwa katika maeneo tofauti waliyopewa wakimbizi wa ndani.

Msaada wa chakula umeanza kutolewa

Kulingana na sekretarieti ya kudumu ya Baraza la Kitaifa la Usaidizi wa Dharura, zaidi ya tani 250 za chakula na wanyama kadhaa pia walisombwa na maji. Watu walioathirika wanahitaji msaada wa chakula. Watu 11,000 tayari wamepokea misaada watakayotumia kwa kipindi cha miezi miwili. Mchele, mtama, mahindi na maharagwe ndivyo wamepewa watu hao kama msaada.

Lakini itakuwa muhimu kujenga upya nyumba, kununua vifaa vya usafi, na kufuatilia afya za wahanga. Kulingana na makadirio ya mpango wa kukabiliana na dharura, mahitaji yanakadiriwa kuwa zaidi ya faranga za CFA bilioni 9. Serikali imetangaza hali ya janga la asili na ikatenga faranga za CFA bilioni 5.