ALGERIA-RSF-HAKI

Hatua ya kumbakiza jela mwandishi wa habari Khaled Drareni yazua taharuki Algeria

Maandamano ya kuunga mkono mwandishi wa habari Khaled Drareni mbele ya majakama ya Algiers Septemba 15, 2020.
Maandamano ya kuunga mkono mwandishi wa habari Khaled Drareni mbele ya majakama ya Algiers Septemba 15, 2020. AFP

Mwanahabari wa Algeria Khaled Drareni, ambaye anazuiliwa jela tangu mwishoni mwa mwezi Machi mwa huu, ataendelea kubaki jela kulingana na hukumu iliyochukuliwa Jumanne wiki hii na Mahakama ya Rufaa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama ya Rufaa nchini Algeria ilimhukumu mwandishi huyo kifungo cha miaka miwili jela kwa kutaka kuhatarisha usalama wa taifa na kuleta uchochezi kwa kuhamasisha kundi lisilo na silaha.

Hukumu hii kubwa aliyopewa mwandishi wa shirika la wanahabari wa Wasio na Mipaka (RSF) na TV5 Monde pia mkurugenzi wa Gazeti la Casbah Tribune nchini Algeria, inaendana na matakwa ya mamlaka ambayo inataka kusiwepo na mtu mwengine atakaye thubutu kuingia mitaani sawa na maandamano yaliyosababisha kujiuzulu kwa rais Abdelaziz Bouteflika mwaka Aprili 2019, kulingana na mashirika ya haki ya binadamu.

RSF imelaani uamuzi "wa kipuuzi na ulio kinyume na sheria" na kutangaza kwamba miji mikubwa kadhaa ya Ufaransa, ikiwa ni pamoja na ule wa Paris kuanzia jana Jumanne jioni, wanatarajia kuweka turubai kwenye viunga vya kumbi za miji yao ili kuonyesha uungwaji wao mkono kwa mwandishi huyo.

Khaled Drareni alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani mwezi uliopita. Mwanahabari huyo, ambaye kwa zaidi ya mwaka mmoja alitoa habari zinazohusiana na maandamano ya kila wiki ya vuguvugu la "Hirak" dhidi ya utawala ulioko madarakani, alikamatwa mwezi Machi mwaka huu.

Maandamano haya yalilazimika kusitishwa kwa sababu ya janga la Corona lakini wanaharakati wengine wametoa wito yarejeshwe wakati masharti yaliyowekwa kudhibiti ugonjwa huo hatari yataondolewa.

Waandamanaji wa vuguvugu la "Hirak" wanadai wajiuzulu vigogo walioko madarakani wakisaidiwa na jeshi na badala yake kurejelewa kwenye nyadhifa zao na kizazi kipya cha viongozi.