AFRIKA KUSINI-CORONA-AFYA

Utafiti: Watu Milioni 12 wambukizwa virusi vya Corona Afrika Kusini

Afrika Kusini inaongoza kwa maambukizi ya virusi vya Corona Afrika.
Afrika Kusini inaongoza kwa maambukizi ya virusi vya Corona Afrika. REUTERS/Siphiwe Sibeko/File Photo

Utafiti wa watalaam wa afya nchini Afrika Kusini, umebaini kuwa watu Milioni 12 waliambukizwa virusi vya Corona, katika taifa hilo ambalo limeongoza kwa maambukizi barani Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Zweli Mkhize amesema utafiti huo mpya unakadiria kuwa, watu milioni 12 ambao ni sawa na  asilimia 20% ya idadi ya watu nchini humo, huenda tayari wameambukizwa virusi  hivyo, katika nchi hiyo ambayo ina maambukizi zaidi ya Laki Sita.

Utafiti huo unaonesha kuwa idadi halisi ya maambukizi inaweza kuwa kubwa zaidi, kati ya 35% na 40%, na watu waliaothirika zaidi ni wale wanoishi katika maeneo ambayo kuna watu wengi.

Hata hivyo, kupungua kwa maambukizi katika siku za hivi karibuni kumezua maswali kuhusu kiwango cha kingamwili kwenye damu ya wagonjwa waliopimwa.

Mwezi Julai, kati ya kesi mpya 10,000 na 15,000 ziliripotiwa kila siku. Lakini katika saa 24 ziliyopita, kesi mpya 956 tu ndizo zilizoripotiwa.

Rais Cyril Ramaphosa ametarajiwa kukutana na washauri wake kuhusu janga hili, huku ikitarajiwa kuwa huenda akafungua zaidi nchi hiyo baada ya visa vya maambukizi kuanza kupungua.