Msumbiji-USALAMA-HAKI

Video ya mauaji yanayohusishwa wanajeshi yaibua maswali mengi Msumbiji

Machafuko Kaskazini mwa Msumbiji tayari yamegharimu maish ya watu 1,500 na zaidi ya 250,000 wamehama makazi yao.
Machafuko Kaskazini mwa Msumbiji tayari yamegharimu maish ya watu 1,500 na zaidi ya 250,000 wamehama makazi yao. Emidio JOSINE / AFP

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limetaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu mwanamke mjamzito aliyeuawa akiwa uchi na wanaume waliovaa sare za jeshi Kaskazini mwa Msumbiji, ukatili ambao serikali imenyooshea kidole cha lawama waasi wenye silaha.

Matangazo ya kibiashara

Picha za video zilisambaa mitandaoni zikiwaonesha wanaume waliovaa sare za jeshi wakimpiga mwanamke huyo wakimshutumu kuwa mwanachama wa kundi lenye silaha, na baadaye kumpiga risasi mara 36 mgongoni alipojaribu kukimbia.

Aidha, video hiyo inaonesha wanaume hao wakimpiga kichwani na mwilini mwanamke huyo kwa fimbo kisha wengine wakammiminia risasi katika tukio lililofanyika katika mkoa wa Kaskazini wa Cabo Delgado, ambapo wanajeshi wa serikali wanapambana na waasi wenye silaha.

Waziri wa mambo ya ndani Amade Miquidade amesema wauwaji hao ni wapiganaji wenye silaha ambao walivalia sare zinazofanana na zile za wanajeshi wa serikali.

Jeshi la Msumbiji limelaani tukio hilo la kutisha na kusikitisha, na kusema ni ukiukwaji wa haki za binadamu wakati huu linapoendeleza makabiliano dhidi ya makundi yenye silaha, Kaskazini mwa nchi hiyo.