MALI-ECOWAS-SIASA-USALAMA

Wanajeshi wanaoshikilia madaraka Mali watathmini ombi la ECOWAS

Assimi Goita, rais wa Baraza la Kitaifa la Wokovu la Watunchini Mali (CNSP), wakati wa mkutano wa ECOWAS huko Accra, Septemba 15, 2020.
Assimi Goita, rais wa Baraza la Kitaifa la Wokovu la Watunchini Mali (CNSP), wakati wa mkutano wa ECOWAS huko Accra, Septemba 15, 2020. Nipah Dennis / AFP

Siku moja baada ya mkutano wa kilele wa Accra, ambapo ujumbe wa kundi la wanajeshi wanaoshikilia madaraka nchini Mali ulikwenda kukutana na ujumbe wa wakuu wa nchi za ECOWAS, maafisa kutoka kundi hilo wameanza kukutana.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa kundi hilo ambaye alishiriki mkutano huo nchini Ghana ameanza kukutana na maafisa wenzake, saa chache tu baada ya kurejea nchini Mali usiku wa Jumanne Septemba 15 kuamkia Jumatano Septemba 16.

Kiongozi huyo amewaelezea wenzake ombi la Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi.

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi waliwataka viongozi wa kijeshi nchini Mali, kukabidhi madaraka haraka kwa raia, baada ya mazugumzo yaliyofanyika siku ya Jumanne jijini Accra nchini Ghana.

Wakuu wa nchi za ECOWAS, walikuwa wametaka rais wa kiraia kupatikana kufikia jana lakini hilo limegonga mwamba.

Mwenyekiti wa ECOWAS Nana Akufo-Addo, ambaye pia ni rais wa Ghana, amesema hakuna mwafaka wowote uliopatikana na ujumbe wa wasuluhishi utakwenda jijini Bamako wiki ijayo kwa mazungumzo zaidi, huku wakiwa na matumaini kuwa suluhu itapatikana.

Viongozi wa kijeshi nchini Mali walimwondoa madarakani rais Ibrahim Boubacar Keita, na wamekuwa wakipata shinikizo za kurejesha madaraka kwa raia.