LIBYA-SIASA-USALAMA

Libya: Waziri Mkuu Fayez el-Sarraj kuachia ngazi mwishoni mwa mwezi Oktoba 2020

Waziri Mkuu wa Libya Fayez el-Sarraj, Aprili, 2016 à Tripoli.
Waziri Mkuu wa Libya Fayez el-Sarraj, Aprili, 2016 à Tripoli. AFP/Mahmud Turkia

Katika hotuba yake kwenye televisheni, Waziri Mkuu wa Libya Fayez el-Sarraj ametangaza kwamba ataachia ngazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyo wa Libya, ambaye yuko madarakani tangu mwezi Machi 2016, anaongoza Serikali ya umoja wa kitaifa, halali na inayotambuliwa na jamii ya kimataifa lakini inapingwa na mbabe wa kivita Mashariki mwa Libya Marshal Khalifa Haftar na vikosi anavyoongoza.

Hivi karibuni serikali ya Tobruk iliamua kujiuzulu, baada ya kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa bunge la nchi hiyo, baada ya siku nne za maandamano ya watu wenye hasira kutokana na uhaba wa bidhaa mahitajio na kuzorota kwa huduma za umma.

Hatua ya kujiuzulu kwa serikali ya mpito inayoongozwa na Abdallah al-Thani ilitangazwa kufuatia mwito wa dharura uliyotolewa kwa serikali na Aguila Saleh , spika wa Bunge lenye makao yake huko Tobruk.

Kujiuzulu huko kunakuja baada ya maandamano ya siku nne mashariki mwa Libya dhidi ya hali duni ya maisha ya kiuchumi na kijamii. Maandamano haya yalianza huko Tripoli na magharibi mwa nchi mwezi uliopita.