ALGERIA-MALI-SIASA-USALAMA

Algeria yatiwa wasiwasi na hali ya usalama nchini Mali

Waziri wa Mambo ya nje wa Algeria Sabri Boukadoum, Julai 13, 2020.
Waziri wa Mambo ya nje wa Algeria Sabri Boukadoum, Julai 13, 2020. AFP Photo/FETHI BELAID

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Sabri Boukadoum anazuru nchi ya Mali tangu Jumapili Septemba 21, ikiwa ni ziara yake ya pili katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Matangazo ya kibiashara

Waziri huyo wa Algeria amekutana kwa mazungumzo na kiongozi wa kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali, Kanali Assimi Goïta. Amekuja kuwasihi viongozi wa kijeshi wanaopshikilia madaraka nchini humo kujikita hasa katika utekelezajiwa mkataba wa amani wa mwaka 2015.

Agosti 28, Sabri Boukadoum alikuwa kiongozi wa kwanza wa serikali ya kigeni kukutana na wawakilishi wa kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali kando na wapatanishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria anarudi Bamako kwa wakati muhimu: katika mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuundwa taasisi za mpito.

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari kutoka wizara yake, amerudi nchini Mali kusema kuwa nchi yake iko "tayari" "kuunga mkono" Mali katika juhudi zake za mabadiliko kwa njia ya "utulivu na amani".

Lakini kulingana na chanzo cha kidiplomasia kutoka Umoja wa Afrika, hali ya usalama na hasa utekelezaji wa mkataba wa amani wa mwaka 2015 ndivyo vinawatia wasiwasi viongozi wa Algeria.