Bah N'Daw ateuliwa kuongoza serikali ya mpito nchini Mali
Imechapishwa:
Uongozi wa kijeshi nchini Mali, umewataja viongozi wa serikali ya mpito hatua inayokuja kufuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, na Jumuiya ya Kimataifa, kutaka jeshi kukabidhi madaraka kwa raia.
Akiwahotubia wananchi wa Mali kupitia runinga ya taifa kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita ametangaza kuwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Bah N'Daw, atakuwa rais wa mpito, huku yeye akiwa naibu wake.
Hatua hii imekuja baada ya mkutano wa wiki iliyopita kati ya wanajeshi nchini Mali na viongozi wa ECOWAS ambao wameiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi ya Mali, kama njia mojawapo ya kuharakisha uteuzi wa raia kuongoza serikali hiyo.
Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa uteuzi wa Bah N'Daw, mwenye umri wa miaka 70 na mwanajeshi wa zamani, ni ishara kuwa jeshi nchini humo hawataki kuachia madaraka moja kwa moja baada ya kusema kuwa wanataka kuongoza serikali hiyo ya mpito.
Rais huyo wa mpito alihudumu kama Waziri wa Uinzi chini ya rais wa zamani Ibrahim Boubakar Keita aliyeondolewa madarakani mwezi Agosti na anatarajiwa kuongoza kwa muda wa miezi kumi na minane kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Uteuzi wake umezua maoni mbalilbali katika taifa hilo la Afrika Magharibi kutoana na uhusiano wake na wanajeshi.